1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ya uhaba wa maji safi ya kunywa katika India

13 Agosti 2007

Mvuwa za masika zimeshika kasi hivi sasa nchini India. Haya ni maafa yanayoonekana kila mwaka. Mafuriko ya maji yametanda vijijini na katika mashambani, huku mawimbi ya maji hayo yalio manjano yakienda kwa kasi za dhoruba katika barabara za miji.

https://p.dw.com/p/CHjm
Maji ya mvuwa ya Masika katika Bwawa la Kadana, kusini mwa Ahmadabad, mkoa wa Gujarat, India.
Maji ya mvuwa ya Masika katika Bwawa la Kadana, kusini mwa Ahmadabad, mkoa wa Gujarat, India.Picha: AP

Mnamo miezi mitatu peke yake kunanyesha asili mia 80 ya mvuwa ya mwaka mzima. Lakini bila ya mvuwa za masika, India, ilio na wakaazi bilioni 1.1 itakumbwa na njaa. Mvuwa hizo zinawaingiza watu katika maafa ya mafuriko, kama vile tunavoshuhudia sasa. Na japokuwa yaonekana kuna maji ya kutosha, kile kinachokosekana ni maji safi ya kunywa. Pia maji hayo yanagawika sio kwa njia yenye kuaminika mnamo kipindi cha mwaka. Jee miradi mikubwa ya serekali ya India inaweza kuinusuru hali ya sasa?

Mara nyingine mvuwa za masika zinaleta baraka, lakini mara nyingine zinaleta balaa. Hivyo ndivyo zilivyo mvuwa za masika. Kuna maeneo mengine yanayobarikiwa kwa kupata mvuwa nyingi, lakini maeneo mengine huambulia mvuwa chache. Sio mawingu yalio juu ndio sababu ya maafa, bali wanadamu pia wanabeba dhamana kwa India kuwa na tatizo kubwa la maji. Mito na mabwawa mengi ya nchi hiyo ni machafu sana, na maji yake hayawezi kutumika. Na kote kunapungua hifadhi za maji ya chemchem kutoka ardhini. Ndio maana mizozo inayosababishwa na kupunguwa sana hifadhi za maji inazidi. Siku za mbele India itahitaji maji zaidi ili kutosheleza mitaa yake ya mijini, kwa ajili ya shughuli za viwanda na kwa ajili ya kuzalisha vyakula kwa wakaazi wak ambao idadi yao inazidi kuengezeka.

Dawa ya hali hiyo ni miradi kabambe ya kupata maji ambayo inapangwa kuanzishwa na wizara ya maji na itahusu kuwa na mtandao wa mifumo ya mito katika nchi hiyo. Kwa msaada wa mbwawa, mito inayokwenda kwa kasi kutokea Milima ya Himalaya itazuiliwa, na maji yake kuongozwa katika mifereji yenye urefu wa kilomita 1000 kuelekea kusini mwa nchi hiyo. Hiyvo mafuriko yanayotokea kaskazini mwa nchi hiyo yatapungua na njaa inayotokea mara nyingi sehemu za Kusini itazuilika.

Mhandisi M.G. Padhye aliyestaafu, aliyewahi kutumika kama katibu mkuu katika wizara ya maji ya India katika miaka ya thamanini na ambaye aliongoza uchunguzi wa mradi huo anasema:

+Tumegundua kwamba kuna mto unatoa maji mengi, na kuna mwengine unaotoa maji kidogo kuweza kutosheleza mahitaji ya watu. Kimsingi tunayazuwia maji ziyada ambayo ama sivyo yangemwagikia baharini, katika mabwawa na kuyaongoza katika mifereji katika miaeno makavu. Pale mradi huo utakapofaulu, tutakuwa na ziyada ya asilimia 25 ya maji tutakayoweza kuyatumia, na hivyo kuweza kunyunyuzia hektari milioni 35 za ardhi ya kilimo+

Mikoa mwili imeshatia saini mapatano juu ya kuwezesha mradi huo wa kubadilisha njia inayopitia mito. Kuna serekali nyingine za mikoa ambazo zina wasiwasi na mradi huo, kwani hazitaki maji yao wayagawe na mikoa mingine. Wahakiki wengi, wakiwemo wanasayansi, walinzi wa mazingira na vyama vya wakulima wanaonya kuweko tahadhari, na wanataka ushahidi wa kisayansi kama mradi huo utaleta tija ya kiuchumi.

Himashu Thakker ambaye anauongoza mtandao wa Kusini mwa Asia unaohusu mabwawa, mito na watu, ana wasiwasi mkubwa:

+Kutakuweko na athari mbaya sana kutokana na kuuleta mtandao mmoja wa mito. Utaharibu mito hiyo na kuiangamiza misitu na maeneo ya kilimo. Mamilioni ya watu watahamshwa kutoka maeneo yao, kwani mradi huo utahitaji mamia kwa maelfu ya hektari za ardhi. Maeno ya juu kunakotokea mito hiyo yatakuwa na uhaba wa maji, ardhi itakuwa ya chumvi, uchafu mwingi utaingia katika maji ya mito, na hivyo kuwaangamiza wanyama wanaoishi ndani ya mito.+

Mnamo miaka mia moja iliopita India imejenga mabwawa makubwa 4291 ili kusaidia unyunyizaji wa maji mashambani, kuengeza uzalishaji wa nafaka, hivyo kuifanya nchi hyio iliokuwa zamani inaugua kwa njaa kila wakati iwe nchi yenye kujitegemea katika chakula. Lakini ujenzi wa mabwawa hayo umepelekea watu milioni 40 kuhama kutoka makaazi yao ya asili na kuharibu wizani wa kimazingira katika vijiji vingi.

Bwana Himanshu Thakkar anahoji kwamba kuvitengeneza upya maelfu ya vidimbwi vya maji katika vijiji kunaweza kuchangia katika kupambana na ukame. Kwa ufupi maji ya mvuwa lazima yakingwe na kuhifadhiwa kwenye maeneo mvuwa inakonyesha ili kwamba hifadhi ya maji katika chemchem za maeneo hayo zijae.