1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matayarisho ya kuanza msimu Bundesliga yanaendelea

Sekione Kitojo
29 Julai 2019

Timu  mbali mbali za ligi  ya  Ulaya  zinajitayarisha kwa ajili  ya msimu  ujao, Borussia Dortmund yaikaribisha Bayern hapo Jumamosi kwa ajili ya mchezo wa Super Cup nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/3Muc3
Fußball | Bundesliga 34. Spieltag | Borussia Mönchengladbach - Borussia Dortmund | Tor 2:0
Picha: Getty Images/AFP/L. Kuegeler

Wakati  vilabu  vya  Bundesliga  vikijitayarisha  kwa  msimu  ujao  wa bundesliga, mabingwa  watetezi  Bayern Munich wamo  katika  heka heka  ya  kuimarisha  kikosi  chake, hasa  ushambuliaji  baada  ya wachezaji  wawili  wakongwe   Frank Ribbery  na  Arjen  Robben kuamua  kutundika  madaluga  baada  ya  kuitumikia  klabu  hiyo  kwa zaidi  ya  miaka  11.  Klabu  ya  Bayern imo  katika  mazungumzo  na mshambuliaji  wa  pembeni  wa  Manchester  City  na  timu  ya  taifa ya  Ujerumani  Leroy Sane, na  kwa  mujibu  wa  jarida  la  michezo la  Kicker, mazungumzo  yanaendelea  vizuri na  kumebakia mambo kama  mshahara  na  marupurupu mengine  ambayo Man City itapata kutokana  na  mafanikio  ya  Sane  katika  klabu  hiyo.

Premier League 31. Spieltag | Manchester United vs. Manchester City
Leroy Sane mchezaji wa Manchester City anamazungumzo na Bayern MunichPicha: Imago Images/PA Images/M. Egerton

Hata  hivyo mwishoni  mwa  juma uwanja  wa  Signal Iduna Park mjini  Dortmund  utawaka  moto wakati  Bayern  Munich  mabingwa watetezi wa bundesliga  watakapojitupa uwanjani  kupambana  na wenyeji  wao  Borussia  Dortmund  kuwania  Super Cup nchini Ujerumani , ikiwa  ni  ishara  ya  kufunguliwa  msimu  wa  56  wa Bundesliga.

Waandishi  habari  za  michezo  nchini  Ujerumani  wamemchagua Marco Reus  kuwa  mchezaji bora  wa  mwaka  katika  Bundesliga, na  kocha  bora  wa  mwaka  amechaguliwa  Juergen Klopp  wa klabu  ya  Liverpool  ya  Uingereza  ambayo  imekuwa  mshindi  wa Champions League barani  Ulaya  mwanzoni  mwa  mwezi  wa  Juni.

Huko  nchini  Uingereza  kocha  wa  Liverpool  Juergen Klopp amekiri  leo  kwamba  kikosi  chake  bado hakija kaa  imara  wakati kikijitayarisha  kwa  ajili  ya  mchezo  wa  mwishoni  mwa  juma  wa kuwania  ngao ya jamii, Community Shield, dhidi  ya  Manchester City. 

Fussball l Marco Reus ist der Fußballer des Jahres
Marco Reus nahodha wa Borussia DortmundPicha: ImagoImages/Kirchner-Media

Mo Salah , Roberto Firmino  na  Alisson  wanarejea  kikosini  kwa ajili  ya  mazowezi  leo  jioni  wakati  Sadio Mane  atakosa  pambano hilo siku  ya  Jumapili katika  uwanja  wa  Wembley  baada  ya kuwamo  katika  kikosi  cha  timu  ya  taifa  ya  Senegal  kilichofikia fainali  ya  kombe  la  mataifa  ya  Afrika  AFCON mwezi  huu.

"Sitaki kutafuta  visingizio  kabla  ya  kucheza  na  Man City  lakini tumekuwa  katika  matayarisho  ya  kabla  ya  msimu  bila  wachezaji sita," Klopp  aliwaambia  waandishi  habari. "Siwezi  kulibadili  hilo. Siwezi  kusema  tumekuwa  na   wakati bora  kabisa  wa matayarisho ya  kabla  ya  msimu, tumefanya  mazowezi  vizuri  lakini michezo  imekuja  katika  wakati mbaya."

Lakini  Klopp  amesema  kikosi  chake , ambacho kilishinda Champions League  mwanzoni  mwa  mwezi  uliopita , kitakuwa tayari  kukabiliana  na  mabingwa  wa  Premier League  City katika uwanja  wa  Wembley siku  ya  Jumapili.

UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Kocha wa Liverpool Juergen KloppPicha: Reuters/C. Recine

"Sifikiri  kwamba  tutacheza mchezo wetu  bora  siku  ya  Jumapili, lakini  ni  suala  la  ushindi," ameongeza.

"Tukishinda  tukishindwa , haitakuwa  na  athari  katika  ligi." amesema  Klopp.

"Kitu nilichokiona hadi sasa , ni  kwamba  Manchester wako  vizuri" ameongeza  Klopp.