1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka 2 wa Kijerumani wakombolewa Yemen

18 Mei 2010

Wasichana wawili wa Kijerumani waliozuiliwa mateka kwa takriban mwaka mmoja katika eneo la milimani,kaskazini mwa Yemen wameokolewa kwa msaada wa vikosi vya usalama vya Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/NRBz
Bild 3. Westerwelle Porträt Titel: Guido Westerwelle Beschreibung Guido Westerwelle am Treffen des "Weimarer Dreiecks" in Bonn am 26./27. April 2010.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle.Picha: Marcin Antosiewicz

Ujerumani imefurahi kupata habari za kuokolewa kwa wasichana hao wawili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Guido Westerwelle amesema:

"Tumepumua kuwa raia wetu wawili kutoka jumla ya watu watano waliotekwa nyara nchini Yemen,sasa wapo huru. Lakini bado tuna wasiwasi kuhusu mateka wengine na tutafanya kila kitu ili tupate habari zaidi kuhusu hatima yao."

Westerwelle akaongezea kuwa wasichana hao wawili wanatazamiwa kurejea Ujerumani kesho Jumatano. Lakini hatima ya wazazi wao na mtoto mchanga wa kiume wa mwaka mmoja haijulikani.

Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia, Jenerali Mansour al-Turki, wasichana hao wenye umri wa miaka mitatu na mitano, wamepelekwa hospitali nchini Saudia. Hali yao ni nzuri lakini wanataka kuhakikisha kuwa wasichana hao wataweza kupata huduma za tiba ikihitajika. Taarifa ya wizara hiyo imesema,wasichana hao wawili wa Kijerumani waliokolewa siku ya Jumatatu katika eneo la mpakani, baada ya vikosi vya Saudi Arabia kuwasiliana na wenzao wa Yemen.

Wasichana hao walikuwa katika kundi la Wajerumani saba, mwanaume mmoja wa Kingereza na raia wa kike wa Korea ya Kusini. Kundi hilo lilitekwa nyara katika eneo la milimani, kaskazini mwa Yemen katika mwezi wa Juni mwaka uliopita. Kundi hilo lilihusika na hospitali inayoongozwa na Kanisa la Kiprotestanti mjini Saada, kaskazini-magharibi ya Yemen - eneo linaloshuhudia mapambano ya muda mrefu, kati ya vikosi vya serikali na waasi wa madhehebu ya Kishia ya Zaidi.

Muda mfupi tu baada ya kundi hilo kutekwa nyara, kulipatikana maiti za wanawake 2 wa Kijerumani waliokuwa wauguzi na wanafunzi wa Biblia pamoja na maiti ya Mkorea wa Kusini. Jenerali Turki amesema, hana habari yo yote kuhusu mateka wanne wengine, lakini aliashiria kuwa operesheni ya wapelelezi na vikosi maalum vya Saudi Arabia inaendelea.

Wakati huo huo, ndugu wa familia ya Wajerumani waliotekwa nyara anasema, kuna hofu kuwa mtoto wa kiume aliekuwa na umri wa mwaka mmoja huenda ikawa amefariki. Hata hatima ya Mwingereza alietekwa nyara wakati huo, haijulikani.

Mwandishi: P.Martin/AFPE/ZPR

Mhariri: M-Abdul-Rahman