1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo mapya ya ndege iliyoptea

Admin.WagnerD20 Machi 2014

Serikali ya Australia inachunguza kuhusu vipande viwili vinavyodhaniwa kuwa ni mabaki ya ndege ya Malaysia iliyopotea ikiwa na abiria karibu wiki mbili zilizopita. Vipande hivyo vimeonekana katika eneo la bahari ya Hindi

https://p.dw.com/p/1BT7u
Malaysia Suche Australien Satellitenaufnahme 20.03.2014
Picha za satelite za mabaki yanayodhaniwa kuwa ya ndege ya Malaysia iliyopoteaPicha: Reuters/Australian Maritime Safety Authority

Ndege nne za wachunguzi zimepelekwa katika maeneo ya mbali ya kusini mwa bahari ya Indi kwa lengo la kubainisha kama picha hizo zinahusiano na ndege ya Malaysia iliyopotea wakati huu ambapo ndugu na jamaa wa abiria wakisubiri taarifa za ndege hiyo.

Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott ameliambia bunge la nchi hiyo taswira hizo zinawakilisha taarifa mpya na za kuaminiki lakini alisisitiza mpaka sasa bado haijaweza kubainika moja kwa moja kwa vipande hivyo vina uhusiano na ndege hiyo iliyopotea aina ya MH370. "Mamlaka ya usalama wa majini nchini Australia imepata taarifa kupitia taswira za satelite ya vitu ambavyo vinawezekana vinauhusiano na msako. Kufuatia uchambuzi wa kitaalamu kutoka katika picha hizo za satelite, vitu hivyo viwili vinavyohusika na msako vimeweza kutambuliwa". alisema na waziri mkuu huyo.

Ndege ya Malaysia, Boeng 777, iliokuwa na abiria 227 na wahudumu 12 ilitoweka mapema Machi 8, baada ya kubadilisha muelekeo wa safari kuelekea bahari ya kusini mwa China wakati ilipaswa ielekee Beijing. Sababu ya mabadiliko hayo mpaka sasa bado hazijaweza kufahamika ingawa wachunguzi wanasema kulitokana na kitendo cha makusudi kilichofanywa na mtu aliyekuwemo katika ndege hiyo.

Malaysia Airlines Boeing 777
Ndege ya Malaysia aina ya Boeng 777Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa ya mamlaka ya usalama

Afisa wa Mamlaka ya Usalama Majini nchini Australia (AMSA), John Young amesema vitu hivyo viliwili vikubwa vimebainika kuwa na urefu wa mita 24. Vyote kwa pamoja vimebainika katika eneo la kusini mwa bahari ya hindi , umbali wa kilometa 2,500 kusini mashariki mwa Perth.

Afisa hiyo pamoja na kuiita hatua hiyo kuwa kubwa kufikiwa kwa wakati huu, aliongeza kusema wanapaswa kwenda katika eneo hilo,kuvitafuta, kuviangalia,kuvichunguza ili kuweza kujua kama kweli vitasaidia utafutaji wa ndege hiyo au la.

Hata hivyo waziri mkuu wa Australia ametahdharisha kwamba inawezekana pia uchunguzi huo ukabaidili muelekeo kwa kutokuwa na uhusiano na ndege hiyo.

Jitihada za kimataifa za kuitafuta ndege hiyo zimekuwa zikishindwa kubainisha ukweli lakini picha hizi za sasa za satelite zinaonekana hatua ya kwanza madhubuti katika uchunguzi huo baada ya jitihada zake kuongeza katika eneo hilo la bahari ya Hindii.

Habari za hatua hii ya sasa zimekuwa zikifuatiliwa kwa makini nchini China kwa kuwa theluthi mbili ya abiria walikuwemo katika ndege hiyo ni raia wa taifa hilo.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman