1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya amani ya mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou19 Mei 2009

Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya rais Obama na waziri mkuu Netanyahu mjini Washington

https://p.dw.com/p/HtIu
Rais Obama azungumza na waziri mkuu NetanyahuPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani na waziri mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel wamebainisha hadharani hitilafu zao za maoni kuhusu amani ya Mashariki ya kati na suala la Iran,wakiridhia machache tuu ili wasije wakakorofisha uhusiano wa kihistoria wa nchi zao,tangu siku ya kwanza ya mazungumzo yao.

Benjamin Netanyahu hajaitika mwito wa rais Barack Obama wa kuundwa dola la Palastina.Amesema hata hivyo "anafikiria njia" itakayowawezesha waisrael na wapalastina kuishi kama majirani.

Kwa upande wake rais Barack Obama ameonyesha amepania kutanguliza mbele diplomasia katika suala la Iran,licha ya hofu za Israel,akitangaza mwishoni wa mwaka huu wa 2009 kua ndio muda wa kutathmini kama juhudi hizo za kidiplomasia zimefanikiwa au zimeshindwa.

"Nnaamini ni kwa masilahi sio tuu ya wapalastina,bali pia ya Israel,ya Marekani na jumuia ya kimataifa kufikia ufumbuzi wa madola mawili ambapo wa-Israel na wa-Palastina wataishi kwa pamoja kwa amani na usalama.Hakuna maendeleo yaliyofikiwa upande huo na nimemkumbusha waziri mkuu aitumie fursa ya kihistoria inayojitokeza wakati wa utawala wake."

Rais Obama amesisitiza waisrael na wapalastina wanabidi watilie maanani ipasavyo makubaliano yote yaliyofikiwa na hasa ujenzi wa maeneo ya wahamiaji wa kiyahudi lazma ukome" amesema.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ana msimamo mmoja na rais Obama linapohusika suala la kuendelezwa utaratibu wa amani,akihakikisha "yuko tayari kuanzisha mazungumzo tangu sasa na wapalastina".Amekwepa lakini kuzungumzia dola la Palastina.

Waziri mkuu wa Israel amesema:

"Nnakubaliana na wewe sana katika suala la kuupa msukumo utaratibu wa amani na niko tayari kuanza moja kwa moja mazungumzo pamoja na wapalastina.Nnapendelea kupanua uwanja wa amani kwa kuzijumuisha nchi nyengine za kiarabu.Nnataka kusema wazi hapa,hatutaki kuwatawala wapalastina.Tunataka kuishi kwa amani pamoja nao.Maridhiano yatahitajika kutoka pande zote mbili.Sisi tuko tayari kutekeleza jukumu letu,tunataraji wapalastina watakua pia tayari kutekeleza jukumu lao."

Waziri mkuu wa Israel amesisitiza mpango wa kinuklea wa Iran ambao Israel inaamini umelengwa dhidi yake,unawatia wasi wasi.Anahofia kwamba siasa ya rais Obama ya kuwanyooshea mkono wairan inaweza kuwapatia muda wairan wa kujitengenezea bomu la kinuklea.

Rais Obama amemhakikishia mgeni wake kwamba usalama wa Israel, "dola huru la kiyahudi" ni muhimu kupita kiasi kwa Marekani.

Viongozi wa utawala wa ndani wa Palastina wameyataja matamshi ya rais Obama kua ni ya kutia moyo kinyume na yale ya waziri mkuu wa Israel wanayosema ni ya kuvunja moyo.

Hamas wao wanasema "matamshi ya rais Obama ni maneno matupu tuu."

Nchini Israel kwenyewe,mbunge wa chama cha upinzani cha Kadima Zeev Boim anasema Netanyahu ameshindwa kuitumia fursa iliyojitokeza ya kuanzisha uhusiano wa kuaminiana pamoja na rais wa Marekani.

Mwandushi:Hamidou Oumilkheir

Mhariri:Abdul Rahman