1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

020910 Washington Nahost

Josephat Nyiro Charo3 Septemba 2010

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miaka 2 Waisraeli na Wapalestina wameanza tena mazungumzo ya amani ya ana kwa ana mjini Washington, Marekani

https://p.dw.com/p/P39C
Hillary Clinton (katikati) Benjamin Netanyahu (kushoto), na rais Mahmoud Abbas (kulia)Picha: picture-alliance/dpa

Kabla kuanza mazungumzo hayo, rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchel na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, walikutana katika wizara ya ndani mjini Washington.

Matokeo ya kwanza ya mazungumzo ya mjini Washington ni waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas kuahidi kufanya duru ya pili ya mazungumzo Septemba 14 na 15, ambayo huenda yakafanyika katika mji wa kitalii ya Misri, Sharm el Sheikh ulioko katika bahari ya Shamu. Maandalizi ya mkutano huo tayari yameanza. Rais wa Marekani Barack Obama hatahudhuria mkutano huo, lakini Marekani itawakilishwa na waziri wa mambo ya kigeni Hillary Clinton na mjumbe wake maalum wa Mashariki ya Kati, George Mitchel. Rais Abbas na waziri mkuu Netanyahu watakuwa wakikutana ana kwa ana kila baada ya wiki mbili.

Akiyafungua tena rasmi mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Palestina, Bi Clinton, amesema anafahamu wasiwasi uliosababishwa na miaka mingi ya mzozo na kudamazwa kwa matumaini. Amewaambia rais Abbas na waziri mkuu Netanyahu kuwa, "Kwa kuwa hapa leo mmechukua hatua muhimu ya kuwakomboa raia wenu kutokana na pingu za kihistoria tusiyoweza kuibadili, na kusonga mbele kuelekea amani na heshima ambayo ninyi pekee ndio mnaoweza kuileta."

Bi Clinton amewataka Waisraeli na Wapalestina wawe wavumilivu na wasaidie juhudi za amani zifaulu kwa kuwa mustakabali wao umo mikoni mwao.

Hapo kabla waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amewataka Wapalestina waitambue Israel kama taifa huru la Wayahudi na hitaji la usalama la Israel. Amemwambia rais Abbas kuwa, "Rais Abbas nafahamu fika na naheshimu ari ya wananchi wako kutaka uhuru. Naamini inawezekana kuiainisha ari hiyo na hitaji la Israel la usalama. Ni nafasi ambayo haijawahi kutokea ya kuweza kuumaliza mzozo wa karne. Shalom. Salaam. Amani."

Sarkozy aahidi kusaidia

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amezihimiza Israel na Palestina kuepukana na vitendo vya uchokozi vitakavyoyahatarisha mazungumzo ya amani. Sarkozy ameapa kuusadia mchakato wa amani kutumia miradi imara, pengine kwa kupendekeza kufanya mkutano wa kilele, wakati wa mkutano wa Muungano wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia mwezi Novemba mwaka huu.

USA Frankreich Nicolas Sarkozy bei Barack Obama in Washington
Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, kushoto, na rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama amempigia simu rais Sarkozy na kumshukuru kwa kuahidi kushirikiana naye pamoja na viongozi wengine kuuendeleza mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Taarifa ya ikulu ya Marekani imesema Obama alishauriana na rais Sarkozy kuhusu hatua zinazopasa kufuata ili kuimarisha mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na mamlaka ya ndani ya Wapalestina.

Kitisho cha Hamas

Wakati huo huo, makundi ya wanamgambo katika Ukanda wa Gaza yametangaza kuungana na kuongeza mashambulio dhidi ya Israel yatakayojumulisha pia mashambulio ya kujitoa muhanga. Kwenye mkutano wa hadhara wa kupinga juhudi za amani uliofanyika huko Gaza, msemaji wa kundi la Hamas, Abu Ubaida, amesema makundi 13 yatafanya mashambulio makali dhidi ya Israel mahala popote wakati wowote. Kundi la Hamas limedai kuwaua walowezi wanne wa Kiyahudi na kuwajeruhi wengine wawili ndani ya wiki hii huko Ukingo wa Magharibi.

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Nancy Pillay, amelaani vikali mashambulio hayo akisema wauaji wanaotaka kuyakwamisha mazungumzo ya amani wanaweza kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Mwandishi: Bergmann, Christina (DW Washington)/ZPR/Josephat Charo

Mhariri: Mwadzaya, Thelma