1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini yanatoweka kuwapata walionusurika katika ajali Comoro.

Sekione Kitojo1 Julai 2009

Waziri wa ushirikiano wa kimataifa wa Ufaransa amemtembelea msichana wa miaka 14 aliyenusurika katika ajali ya ndege hospitali hii leo.

https://p.dw.com/p/If3x
Kijana Bahia Bakari msichana ambaye amenusurika , akiwa amezungukwa na madaktari wakati akiwa hospitali.Picha: AP

Waziri wa ushirikiano wa kimataifa wa Ufaransa Alain Joyandet amemtembelea hospitalini msichana wa miaka 14, ambaye ndie pekee aliyenusurika hadi sasa katika ajali ya ndege ya shirika la ndege la Yemen katika visiwa vya Comoro.Hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu watu wengine walionusurika.

Jana Jumanne maafisa wa Comoro walisema kuwa maiti tano zilipatikana kutoka baharini ambako ndege chapa Airbus A 310 ilianguka ikiwa na abiria 153 . Lakini taarifa zilizopatikana leo zinasema kuwa maiti hizo zilionekana zikielea baharini na kwamba waokoaji wamefanikiwa kupata maiti hizo hii leo.

Moja kati ya visanduku vyeusi, ambavyo ni vyombo vya kurekodia mawasiliano kati ya rubani na viwanja wa ndege kimefahamika kilipo na juhudi za kukipata zinaendelea.

Ishara za kisanduku hicho zimepatikana jana usiku.

Wakati huo huo kundi la Wakomoro wenye hasira leo wamezuwia kuruka moja ya ndege katika uwanjani wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris. Maandamano hayo yanafuatia kuanguka kwa ndege ya shirika la ndege la Yemen katika visiwa vya Comoro. Waandamanaji hao wanadai kuwa shirika hilo la ndege linatumia ndege zisizo salama katika njia kuelekea Comoro.


Wanatufanya kama mbwa, tunapofika Yemen wanatubadilishia ndege, wanatuingiza kama kwenye mapango.


Shirika hilo la ndege la Yemen limesisitiza leo kuwa lina sera imara kwa ajili ya ukarabati wa ndege zake na kupinga minong'ono kuwa tatizo la kiufundi ndio limesababisha kuanguka kwa ndege hiyo.

Shirika hilo la ndege la Yemen limesema leo kuwa litalipa kwa familia za wahanga Euro 20,000 kama fidia ya mwanzo, wakati likisisitiza kuwa ndege hiyo ilikuwa na viwango vya usalama. Je wale waliopoteza wapendwa wao wanahisi nini kuhusu fidia hii iliyotangazwa na shirika hili la ndege. Anafafanua Salim Himid mkazi wa mjini Paris nchini Ufaransa ambaye ana asili ya visiwa vya Comoro.

Matumaini yanazidi kupotea kuwapata watu walionusurika katika ajali hiyo ya ndege, wakati vikosi vya uokozi vikiendelea na msako baharini kwa ajili ya kutafuta mabaki ya ndege hiyo.


Mwandishi Sekione Kitojo/DPAE.

Mhariri:Abdul-Rahman