1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya wageni katika Afghanistan

Miraji Othman7 Agosti 2010

wanachama kumi wa kikundi cha kimataifa cha madaktari, akiwemo Mjerumani, wameuliwa kwa risasi.

https://p.dw.com/p/OegG
Sabine Heimbach, naibu wa msemaji wa serekali ya UjerumaniPicha: REGIERUNGonline/Bergmann
Huko kaskazini mwa Afghanistan, wanachama kumi wa kikundi cha kimataifa cha madaktari, akiwemo Mjerumani, wameuliwa kwa risasi. Jambo hilo limearifiwa na msemaji wa Jumuiya ya Kikristo yenye kutoa misaada, International Assistance Mission, mjini Kabul, Licha ya Mjerumani, miongoni mwa waliouliwa kuna Muingereza, Wamarekani sita, akiwemo mwanamke, na Wa-Afghani wawili waliokuwa wakalimani. Mwanachama mmoja wa Ki-Afghani katika kundi hilo aliiarifu jumuiya hiyo juu ya shambulio hilo. Wataliban wenye itikadi kali za Kiislamu wamechukuwa dhamana ya shambulio hilo. Msemaji wao, Sajbullah Mudjahid, alitangaza kwamba raia hao wa kigeni walikuwa wanafanya ujasusi kwa niaba ya Marekani na kuwabadilisha watu dini kwa ajili ya Ukrito. Mkuu wa polisi katika mkoa wa Badakhshan, Jenerali Agha Nur Kemtus, amesema yawezekana kwamba kisa hicho ni cha wizi wa kawaida bila ya kushiriki Wataliban. Shambulio hilo lilifanyika Ijumaa iliopita.

Serekali ya Ujerumani imelaani vikali kushambuliwa raia wa kigeni wanaotoa misaada huko Aghanistan. Serekali ya Ujerumani imetaka ipatiwe maelezo ya kina juu ya mauaji hayo ya woga na waadhibiwe wale waliofanya uhalifu huo. Hayo yalisemwa na naibu wa msemaji wa serekali ya Ujerumani, Sabine Heimbach. Alisema kisa hicho kinasisitiza juu ya umuhimu wa kusonga mbele katika kuchangia kuleta utulivu katika Afghanistan. Pia chama cha Kijani na kile cha die Linke vimekasirishwa na kisa hicho. Mkuu wa wabunge wa Chama cha Kijani, Jürgen Trittin, amesema kuuliwa kwa wasaidizi hao kunaonesha vipi Afghanistan ilivyo mbali kuwa nchi ilio tulivu. Mkuu wa chama cha die Linke, Gesine Lötsch, kwa mara nyingine tena, alitaka jeshi la Ujerumani liondoke kwa haraka kutoka Afghanistan.