1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya watalii yazusha wasiwasi Uganda

18 Oktoba 2023

Mauaji ya watalii wawili na mwongozaji wao nchini Uganda yameibua hisia za huzuni na hasira miongoni mwa watu mbalimbali isa hicho huku yakidaiwa kufanywa na waasi wa kundi la ADF.

https://p.dw.com/p/4XgaJ
Uganda Kampala Bombenanschlag auf Kirche verhindert
Maafisa wa usalama wa Uganda wakilinda eneo yalikofanyika mashambulizi ya kigaidi kusini mwa mji mkuu Kampala mnamo mwezi Septemba 2023. Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Kulingana na taarifa za polisi na Mamlaka ya Wanyamapori, watalii hao wawili na mwongozaji wao walivamiwa majira ya saa 12:00 jioni, ambapo walishambuliwa na gari lao kuteketezwa moto.

Kisa hicho kilitokea katika mbuga kuu ya wanyamapori ya Queen Elizabeth magharibi mwa Uganda jirani na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma zaidi: Uingereza yatoa tahadhari kwa raia wake Uganda

Msemaji wa Mamlaka ya Wanyamapori, Bashir Hangi, alisema kuwa watalii hao walikuwa raia wa Uingereza na Afrika Kusini.

Polisi na jeshi la Uganda lilisema mauaji hayo yamefanywa na waasi wa kundi la ADF lenye ngome yake kuu nchini Kongo.

Siku ya Ijumaa (Oktoba 13) uvamizi kama huo ulifanyika ambapo wafanyabiashara wawili na dereva wa lori waliuawa eneo jirani na palipotokea kisa cha Jumanne (Oktoba 17).

Tahadhari ya Museveni

Huku akisifu mafanikio ya majeshi ya Uganda na Kongo katika Operesheni Shujaa ya kuwatokomeza waasi hao, Rais Yoweri Museveni hivi karibuni alitahadharisha kuwa waasi hao wangetafuta namna ya kupenyeza na kurudi Uganda.

Yoweri Musevini to sign anti-LGBT law
Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

"Ninawashauri raia muwaripoti watu wowote musiowajua maeneo ya mpakani." Alisema Museveni.

Soma zaidi: Kundi la ADF lafanya shambulizi Uganda

Ni kwa msingi huu ndipo sasa watu kwenye maeneo ya mpakani wamo katika hofu na mashaka makubwa. 

"Kwa nini jeshi halijaonesha kutilia maanani kuimarisha ulinzi tangu mauaji ya mwezi Juni, ambapo watu 41 waliuawa baada ya waasi hao kuvamia shule ya bweni na kuwateketeza wanafunzi," alisema John Kibego, mkaazi wa Hoima, mji unaopakana na Kongo.

Athari kwa utalii

Utalii ni sekta muhimu kwa uchumi wa Uganda, na habari za mauaji ya watalii hao zinatarajiwa kuwatia mashaka wale waliokuwa wamepanga kuja Uganda kuhusu usalama wao hasa katika mbuga hizo zinazovutia watalii wengi kutokana na uoto asili anuwai na wanyamapori wa kipekee.

Uganda Ölförderung Umwelt Indigene Total
Tembo kwenye mbuga ya taifa ya Uganda.Picha: Jack Losh

Tayari Uingereza imetoa tahadhari kwa raia wake wanaotaka kuja nchini Uganda kufuatia kisa hicho.

Soma zaidi: ICC: Bensouda hakufadhili kundi la waasi wa LRA

Juhudi za kukabliana na kundi hilo la waasi chini ya Operesheni Shujaa katika kipindi cha miaka miwili zinaendelea.

Majeshi hutumia hata ndege za kivita kuwashambulia, lakini wanazidi kuwa hatari kwa kuendesha uvamizi katika nchi hizo mbili.

Mwishoni mwa wiki, Rais Museveni alifahamisha kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kuwa jaribio lao la kutega mabomu katika kanisa moja kati mwa Uganda zilitibuliwa.

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala