1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauritania kufanya uchaguzi Jumapili.

Sekione Kitojo9 Machi 2007

Wamauritania wanamchagua rais wa kiraia siku ya Jumapili ambaye atachukua hatamu za uongozi wa kijeshi ambao umemuondoa madarakani mtawala wa zamani wa kimabavu, ikiwa ni sehemu ya mwisho katika njia kuelekea katika demokrasia katika nchi hiyo masikini katika bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/CHIV

Katika hali ambayo si ya kawaida katika bara la Afrika, jeshi litajiondoa madarakani baada ya uchaguzi huo ili kutoa nafasi kwa kiongozi wa kiraia na kumaliza kipindi cha miezi 19 ya mpito kuelekea demokrasia kipindi kilichoahidiwa na utawala wa kijeshi ambao ulichukua madaraka katika mapinduzi ambayo hayakumwaga damu mwezi wa August 2005 na kumaliza miongo miwili ya utawala wa kimabavu chini ya rais Maaouiya Ould Taya.

Madaraka hayajawahi kubadilishwa kupitia uchaguzi katika kolini hili la zamani la Ufaransa, ambayo historia yake imeambatana na mapinduzi pamoja na tawala za kijeshi tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1960.

Kiasi cha watu milioni 1.1 watawajibika kuweka kura zao katika makasha ili kumchagua mmoja kati ya wagombea 19 wa urais katika uchaguzi ambao unaonekana kuwa ni huru katika karibu miaka 50.

Utawala huo wa kijeshi katika nchi hiyo, imewazuwia wanajeshi wote kugombea nafasi yoyote ili kuhakikisha uwazi katika uchaguzi huo. Hata mawaziri katika utawala wa sasa unaoondoka madarakani hawaruhusiwi kugombea katika uchaguzi huo. Kiongozi wa mapinduzi Ely Ould Mohamed Vall ameahidi utawala safi kabisa.

Utawala unaoondoka madarakani umeonyesha wazi kabisa kuwa kati kwa kati. Na hii pia ilikuwa ni maadili ya utawala wa kijeshi.Na hakuna hadi sasa kitu kinachoweza kwenda kinyume na sheria hiyo.

Mbali ya kukosekana kwa maoni ya raia , lakini kiasi cha wagombea watatu hadi sasa wanaonekana kuwa wanauwezo mkubwa wa kushinda uchaguzi huu katika kundi hilo kubwa la wagombea.

Ahmed Ould Daddah , mwenye umri wa miaka 65 ambaye ni mwanasiasa mpinzani mkubwa tangu alipoanza kumpinga rais wa zamani Ould Taya mwaka 1992, ameshindwa mara mbili katika chaguzi mwaka 1992 na 2003. Daddah aliwahi kukamatwa mara kadha kwa kupinga sera za rais Taya. Sidi Ould Chikh Abdellahi mwenye umri wa miaka 69 , mchumi, ambaye aliwahi kuwa waziri mara kadha , anaungwa mkono na watu wengi wanaoumuunga mkono rais wa zamani.

Mwenyekiti wa kambi ya kampeni ya mgombea Ahmed Ould Daddah, Mohammed Mahmoud Ould Oudadi anaelekeza lawama zake kwa utawala wa kijeshi ambao majina yao hakutaka kuwataja kuwa utawala huo haukuwa safi.

Mtu anaweza kwa kiasi fulani kusema, kuwa watu hawa hawako kati kwa kati, kuhusiana na wagombea maalum kutoka katika vyama mbali mbali. Tunampambana kwa pamoja na wagombea wengine dhidi ya baadhi ya wagombea.

Gavana wa zamani wa benki kuu ya nchi hiyo Zeine Ould Zeidane ni mgombea kijana kabisa kati ya wagombea wote na amejitokeza kwa mara ya kwanza katika siasa akiwa mgombea wa kujitegemea.

Wakati huo huo Mauritania imeilalamikia Libya kutokana na matamshi yake kiongozi wake Muammar Gaddafi , ambapo amewaita Wamauritania kuwa wakabila, na kwamba wanapoteza wakati na uchaguzi wa vyama vingi unaotarajiwa kufanyika hapo Jumapili.

Katika hotuba siku ya Ijumaa kuadhimisha miaka 30 ya kutangazwa kuwa Jamahiriyah, ama jamhuri, ambapo vyama vya kisiasa vilipigwa marufuku , Gaddafi amesema mataifa yanapoteza muda wao na siasa za vyama vingi. Aliitaja Mauritania.