1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa Nje wa Umoja wa Ulaya wakutana Slovenia

28 Machi 2008

Mawaziri wa Nje wa Umoja wa Ulaya wamekusanyika mji mkuu wa Slovenia,Ljubljana kwa mkutano wa siku mbilil.Syria,Urusi,Tibet na Kosovo ni miongoni mwa masuala yaliyopangwa kujadiliwa katika mkutano unaoanza leo hii.

https://p.dw.com/p/DWRm

Mikutano isiyo rasmi hufanywa mwaka mara mbili na mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya,kwa azma ya kujadili mwongozo wa sera za nje za pamoja,bila ya kuwa chini ya shinikizo la kupitisha maamuzi.Mada kuu ya mkutano unaoongozwa na Slovenia ambayo hivi sasa imeshika urais wa Umoja wa Ulaya,inahusika na mustakabali wa eneo la magharibi la Balkan baada ya Kosovo kujitangazia uhuru wake.Lakini matukio ya Tibet na China huenda yakagubika mkutano huo,kwani umma unatazamia tangazo fulani kutoka viongozi hao kuhusu mzozo wa China pamoja na msimamo wa Umoja wa Ulaya juu ya suala la kususia Michezo ya Olimpiki mjini Beijing mnamo mwezi wa Agosti.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier ameshasema kuwa anapinga wito wa kususia michezo ya Beijing.Wakati huo huo,waziri mwenzake wa Ufaransa,Bernard Kouchner amesema kuwa hawezi kuondoa uwezekano wa kiongozi wa nchi yake kususia angalau sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo.

China na Umoja wa Ulaya zina uhusiano wa karibu sana katika sekta ya kiuchumi,kwa hivyo itakuwa vigumu kuiwekea serikali ya Beijing vikwazo vya kiuchumi.Vile vile uhusiano pamoja na China hauwezi kutiwa katika hali ya mvutano kwani China iliyo na kura turufu katika Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inahitajiwa katika migogoro mingi ya kimataifa.

Juu ya hivyo,wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanasema,Ulaya inapaswa kuhifadhi uaminifu wake.Mtu hawezi kubakia kimya,haki za binadamu zinapokiukwa huko Tibet.Huu si wakati wa kujadili vikwazo dhidi ya China.

Kwa hivyo mawaziri wa nje wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya watakubaliana kuimarisha majadiliano ya waziwazi pamoja na China.Vile vile watafuatiliza kwa makini matukio ya Tibet pamoja na ukandamizaji wa maandamano.Kwa hivi sasa vikwazo si suala la kujadiliwa.Lakini katika Bunge la Ulaya sauti zilipazwa kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya China.Rais wa Bunge Hans Gert Pöttering akasema yeye angependa kumkaribisha tena bungeni,kiongozi wa Kidini wa Watibet Dalai Lama.

Mada nyingine muhimu ya mkutano wa mawaziri wa nje, inahusika na mataifa ya eneo la magharibi la Balkan yanayotaka kuingia katika Umoja wa Ulaya.Vile vile kuna mgogoro unaohusika na Kosovo iliyojitangazia uhuru wake kutoka Serbia hivi karibuni.Serbia inakataa kabisa kutambua uhuru wa jimbo lake la zamani lililo na wakaazi wengi wenye asili ya Kialbania.Lakini nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zimeitambua Kosovo kama taifa huru na hivi sasa inasaidiwa kujenga mfumo wa kidemokrasia.

Mawaziri wa Nje wa Umoja wa Ulaya wanataka kuzuia mtengano zaidi wa Waserbia wachache walio kaskazini mwa Kosovo na walio watiifu kwa nchi ya asili yao Serbia. Ni matumaini ya mawaziri hao kuwa uchaguzi wa mwezi Mei ulioitishwa mapema nchini Serbia utaingiza madarakani serikali itakayoelewana vizuri zaidi na nchi za Ulaya.