1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ulinzi wa Marekani, Ujerumani watembelea Afghanistan

14 Machi 2012

Wakati hali ya mambo bado si nzuri nchini Afghanstan baada ya askari wa Marekani kuwaua raia 16 wa nchi hiyo, mawaziri wa ulinzi wa Ujerumani na Marekani wanatembelea nchi hiyo kwa lengo la kukutana na Rais Hamid Karzai.

https://p.dw.com/p/14KJQ
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere (nyuma kushoto), akiwa mjini Kabul.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere (nyuma kushoto), akiwa mjini Kabul.Picha: dapd

Ziara hii ya waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, inafanyika ikiwa ni siku mbili tu baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kuzuru nchi hiyo.

Akiwa ametoka katika mazungumzo nchini Pakistan, de Maiziere amepanga kuonana na waziri mwenziwe wa masuala ya Usalama wa Afghanistan, Abdul Rahim Wardak, pamoja na Rais Karzai katika katika kikao ambacho bado hakijawa wazi.

de Maiziere amesisitiza kuhusu jukumu la nchi yake katika mpango wa kulinda amani nchini Afghanistan ikiwa ni siku mbili tu baada ya baada ya Kansela Merkel kuonyesha shaka dhidi ya mpango wa Ujerumani kuondoa majeshi yake ifikapo mwaka 2014 akisema kuwa bado hali si nzuri kiasi nchini Afghanistan kwa majeshi hayo kuondoka.

Panetta naye yupo Afghanistan

Naye Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta, yupo katika eneo la kusini mwa Afghanistan katika kambi ya kijeshi ya Wamarekani ya Bastion baada kuzuka kwa hofu ya chuki ya Waafghanistani dhidi wanajeshi wa Marekani kufuatia tukio la mauaji ya raia 16 lililofanywa na mwanajeshi mwenzao.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Leon Panetta.Picha: dapd

Wasiwasi umezidi baada ya mtu mmoja anayeshukiwa kuwa ni mfuasi wa kundi la Taliban kurusha risasi kwa ujumbe wa serikali ya Afghanistan uliokuwa ukishiriki mazishi ya watu waliouawa kwa shambulio hilo la raia lililofanywa na mwanajeshi wa Marekani.

Panetta pia kama ilivyo kwa de Maiziere amepanga kuonana na Rais Karzai pamoja na viongozi wa jadi wa maeneo ya kusini mwa nchi hiyo kwa lengo la kuwahakikishia usalama wa Waafghanistan baada ya tukio hilo la mauaji

Mripuko wasikika Kandahar

Wakati ziara hizo za mataifa yenye vikosi vyake vya kijeshi nchini Afghanistani zikijiri, kusini mwa mji wa Kandahar kumesikika mlio mkubwa wa mlipuko wa bomu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, chanzo cha mripuko huo bado hakijafahamika mara moja. Mji huo ndipo mahala ambapo askari wa Marekani alitekeleza mauaji ya raia 16 Jumapili iliyopita.

Marekani ni nchi ya kwanza yenye idadi kubwa ya wanajeshi wake nchini Afghanistani ikifuatiwa na Uingereza huku Ujerumani ikishika namba tatu ikiwa na wanajeshi 4,900. Kati ya hao 52 tayari ambapo mauaji ya wanajeshi 34 yalitokana na chuki ya Waafghanistan dhidi ya majeshi ya kigeni.

Mwandishi: Stumai George/AFPE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman