1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wakuu wa zamani nchini Pakistan washikana mikono

4 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CWTj

ISLAMABAD.Mawaziri wakuu wa zamani wa Pakistan,Nawaz Shariff na Bi Benazir Bhutto wamesema kuwa watatoa orodha ya matakwa yao kwa serikali,yanayowafanya kususia uchaguzi wa mwezi ujayo.

Katika taarifa yao ya pamoja mawaziri wakuu hao wa zamani wa Pakistan wamesema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo wa bunge hapo tarehe 8 January yana dosari.

Nchi hiyo kwa sasa iko katika hali ya hatari iliyotangazwa na Rais Pervez Musharraf.

Hata hivyo wanasiasa hao walisita kutangaza wazi kuwa wataugomea uchaguzi huo na iwapo watashiriki ni kwa makubaliano gani.

Hapo jana tume ya Uchaguzi nchini humo ilimuengua Nawaz Shariff katika uchaguzi huo kutokana na hukumu iliyotolewa dhidi yake mwaka 2000 kwa madai ya utekaji nyara.

Katika kesi hiyo Nawaz Shariff anatuhumiwa kuzuia ndege ya aliyekuwa mkuu wa majeshi wakati huo Pervez Musharraf kutua nchini Pakistan mwaka 1999.Musharraf baadaye alimpindua Shariff.