1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mayweather afuta uwezekano wa kupigana tena na Pacquiao

9 Mei 2015

Baada ya kusema kuwa angeweza kuwa tayari kwa pigano la marudiano na Manny Pacquiao, bondia Mmarekani ambaye hajashindwa pambano lolote Floyd Mayweather Jr ameubatilisha mkondo akimtaja Mfilipino huyo kuwa mwoga

https://p.dw.com/p/1FNJQ
Manny Pacquiao und Floyd Mayweather Jr
Picha: picture-alliance/dpa/M. Nelson

Katika mahojiano yaliyorushwa hewani leo, Mayweather ameleezea kuchukia kuwa Pacquiao alilaumu kushindwa kwake kutokana na maumivu ya bega lake la kulia katika kile kilichoitwa “pigano la karne” mjini Las Vegas.

Pacquiao alishindwa na Mayweather kwa wingi wa pointi katika pigano hilo lililokusanya mapato makubwa zaidi katika historia ya ndondi kabla ya kufanyiwa upasuaji wa kufana kwenye bega lake la kulia siku nne baadaye.

Mayweather amesema hawezi kukubali madai ya Pacquiao, maana alishindwa, na anafahamu mwenyewe kuwa alishindwa.

Mapema wiki hii, Mayweather alisema yuko tayari kumpa Pacquiao fursa nyingine ya kupigana ulingoni mwaka ujao akisema angeweza kuchelewesha uamuzi wake wa kustaafu kutoka mchezo huo. Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 38 amesalia na pigano moja mwezi Septemba kabla ya kustaafu. Na sasa amebadilisa mawazo yake ya kupigana tena na Pacquiao akisema Mfilipino huyo anastahili kukubali kuwa alishindwa. Kuna mashabiki wengi waliohisi kuwa pigano la marudiano lingefaa, lakini sasa kulingana na namna mambo yalivyo, sahau kabisa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu