1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

​​​​​​​Mayweather ambwaga McGregor

Bruce Amani
28 Agosti 2017

Lilitajwa na maafisa walioliandaa, kuwa pigano ambalo mashabiki walitarajia. Pigano la Jumamosi kati ya Floyd Mayweather na Conor McGregor lilihusu kitu kimoja pekee – pesa.

https://p.dw.com/p/2izBD
USA Las Vegas Boxkampf Floyd Mayweather Jr. -  Conor McGregor
Picha: Reuters/S. Marcus

Baada ya kumzidi nguvu McGregor kwa njia ya knockout katika raundi ya 10, Mayweather anaweza kuzitundika glovu zake akiwa na rekodi safi sana ya mapigano 50 bila kushindwa hata moja. Na ametia kibindoni Zaidi ya dola milioni 300..Mmarekani huyo mwenye umri wa miaka 40 ameahidi kutorejea tena ulingoni "sisi sote hufanya mambo ya kijinga lakini mimi sio mjinga. Nikiona fursa ya kutengeneza dola milioni 300, 350 katika dakika 36, mbona nisichukue?. Ilibidi nichukue, lakini hii ni mara ya mwisho, na nnawaahidi hilo. Nimekuwa na taaluma nzuri sana. Siwezi kulalamika kuhusu chochote. Waandalizi wa pigano hili walinipa mkataba mkubwa kabisa katika historia ya mchezo huu"

USA Las Vegas Boxkampf Floyd Mayweather Jr. -  Conor McGregor
McGregor amesema ni wakati wa kutafuta pesa zaidiPicha: Reuters/USA Today Sports/M. J. Rebilas

Mayweather ambaye alistaafu baada ya kumshinda Andre Berto mnamo mwezi Septemba 2015 amesema hakuna kilichosalia kuudhihirishia ulimwengu. Hatahivyo kwa McGregor ambaye ni raia wa Ireland, ni hadithi tofauti. Anasema ndo mwanzo tu wa safari ya kutafuta hela Zaidi "hundi hii iko sawa. hundi hi sio mbaya. nzuri kabisa! lakini, angalia, nimekuwa nikipata hundi kupitia mchezo wangu wa ngumi na mateke hivyo msinichukulie vibaya. Bado ntaendelea kupata hundi hizi wakati ntakaporudi katika mchezo huo

Bondia huyo mwenye umri wa miaka 29 ameanzisha tovuti yake, kampuni ya mavazi, na biashara nyingine kadhaa.

Mayweather alikiri kwamba pigano dhidi ya McGregor lilimchukua muda mrefu kumsimamisha kinyume na alivyotarajia. Lakini naye McGregor ambaye alishiriki kwamara ya kwanza mchezo wa ndondi za kulipwa, alisema refa Robert Byrd alifanya makosa kusimamisha pigano hilo katika raundi ya kumi. Raia huyo wa Ireland ambaye amesema atarudi kuendelea na mchezo wake wa ndondi na mateke – wa Ultimate Fighting Challenge licha ya kusema huenda akarudi tena katika ulingo wa ndondi anasema kuwa alikuwa amechoka kiasi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdulrahman