1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazishi ya Boris Yelzin

Oummilkhheir25 Aprili 2007

Walimwengu na warusi wampa heshma za mwisho rais wa kwanza wa Urusi Boris Yelzin

https://p.dw.com/p/CHFU
Picha: AP

Warusi wamemuandalia maziko makubwa rais wao wa kwanza Boris Yeltzin hii leo wakihudhuria kiongozi wa taifa la Urusi Vladimir Putin ,rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani Horst Köhler ,marais wa zamani wa Marekani,George Bush mkubwa na Bill Clinton na kiongozi wa mwisho wa Usovieti Mikhail Gorbatchev.

Viongozi kadhaa wa dunia na maelfu ya warusi wamempa hishma za mwisho rais wa kwanza wa Urusi Boris Yeltzin aliyefariki dunia jumatatu iliyopita akiwa na umri wa miaka 76.Maiti yake iliyolazwa ndani ya jeneza lililoachwa wazi na kupambwa kwa rangi za bendera ya taifa nyerupe,buluu na nyekundu iliwekwa katika kanisa la muokozi mjini Moscow.

Ilikua mchana tena pale rais Vladimir Putin na viongozi kadhaa mashuhuri kutoka nje walipowasili katika kanisa hilo kuhudhuria misa ya mazishi.

Bill Clinton na mtangulizi wake George Bush mkubwa pamoja na viongozi kadhaa mashuhuri waa dunia walimuamkia kwa dhati mjane wa Yelzin Naina na binti zake wawili,Elena na Tatiana.

Maelfu ya warusi walimiminika kabla ya hapo kuomboleza mbele ya maiti ya kiongozi ambae mwaka 1991 alimaliza enzi za Usovieti na kuifungulia Urusi milango ya mfumo wa kiberali pamoja na machungu yaliyosababishwa na mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.

Rais Vladimir Putin ameitangaza siku ya leo kua ni siku ya maombolezi na bendera zimeshushwa nusu mlingoti katika majumba yote ya serikali yaliyofungwa pia vitambaa nyeusi.

Hii ni mara ya kwanza tangu mapinduzi ya mwaka 1917, kwa kiongozi wa zamani wa Urusi kuzikwa kuambatana na desturi za kanisa la kiorthodox.Na chaguo la kanisa kuu la Muokozi ambalo Yelzin aliamuru lijengwe sawa na lile lililoripuliwa na Stalin mwaka 1931,lina maana maalum.

Vituo vyote vya televisheni vya Urusi vinaonyesha mtindo mmoja,tena tangu jana ibada zinazoongozwa na maaskofu waliovalia mavazi yenye rangi nyesi na nyeupe au hata maombolezi ya wananchi wa kawaida .

Rais wa kwanza wa Urusi Boris Yeltzin amezikwa leo jioni katika kiunga cha NOVODEVITCHI,walikozikwa pia wanasiasa mashuhuri wa Urusi ikiwa ni pamoja na jeneral Alexander Lebed aliyemuunga mkono kukabiliana nawaasisi wa mapinduzi ya Agosti 19 mwaka 1991 dhidi ya Mikhael Gorbatchov na kiongozi wa zamani wa kikoministi NIKITA KHROUCHTCHEV.

.