1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu mzozo wa Yemen yacheleweshwa

18 Aprili 2016

Mazungumzo yaliyonuiwa kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen yaliopangwa kuanza leo (18.04.2016) nchini Kuwait yamecheleweshwa kutokana na mapigano yanayoendelea.

https://p.dw.com/p/1IXdJ
Jemen Kämpfer auf einem Toyota Pick up Patrouille
Picha: picture-alliance/dpa/Stringer

Maafisa wa pande zinazohusika katika mzozo huo wamesema mazungumzo hayo hayatafanyika kama ilivyopangwa huku kukiwa na misimamo tofauti kuhusiana na mapigano yanayoendelea licha ya kutangazwa usitishwaji uhasama.

Ujumbe unaoliwakilisha kundi la Wahouthi na chama cha rais wa zamani wa Yemen, Ai Abdullah Saleh, bado hawajaondoka mji mkuu Sanaa na wamezungumzia mashambulizi makali yanayofanwa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia. "Hakuna haja ya kwenda Kuwait kama mkataba wa kusitisha mapigano hauheshimiwi," amesema afisa wa cheo cha juu wa chama cha General People's Party cha rais Saleh, wakati alipozungumza na shirika la habari la Reuters.

Maafisa wawili wa serikali ya Yemen wamesema wajumbe wa upande wa upinzani wanatarajiwa kuwasili Kuwait kesho Jumanne. "Wajumbe wa chama cha Saleh na waasi wa Houthi wanatafuta sababu kuchelewa kufika kwa wakati unaofaa, lakini inatarajiwa watafika baadaye kesho Kuwait," alisema mmoja wa maafisa hao.

Jemen Aden Demonstration Südjemen Separatisten
Maandamano ya kutaka Yemen Kusini ijitengePicha: Getty Images/AFP/S. Al-Obeidi

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed aliwasili jana Kuwait, ambako alizungumzia hali ya wasiwasi mkubwa inayoikabili Yemen. Hata hivyo alipolihutubia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa iliyopita, Cheikh Ahmed alisema Yemen haijawahi kukaribia hatua ya kupata amani kama wakati huu.

Saudi Arabia na baadhi ya mataifa ya Kiarabu washirika katika eneo la Ghuba walijiunga na vita vya Yemen Machi 26 mwaka uliopita kuiunga mkono serikali baada ya kulazimishwa kukimbilia uhamishoni na waasi wa Houthi na vikosi vilivyo tiifu kwa Saleh.

Mazungumzo ya awali yalifeli

Mazungumzo ya awali yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa mwezi Juni na Desemba mwaka uliopita yalishindwa kuvimaliza vita nchini Yemen ambavyo vimesababisha vifo vya watu 6,200, kiasi nusu yao wakiwa raia. Watu wengine milioni 2.4 wamelazimika kuyahama makazi yao.

Mzozo huo umeruhusu wapiganaji wa mtandao wa al Qaeda kuyadhibiti maeneo na kuwafungulia njia wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu kujiimarisha na kuwa na nguvu nchini humo.

Mapigano na mashambulizi ya kutokea angani yamekuwa yakiendelea katika maeneo mbalimbali kote nchini, hususan katika mji unaozozaniwa wa Taiz, kusini magharibi na eneo la Nehm, mashariki mwa mji mkuu, Sanaa.

Wakati haya yakiarifiwa maelfu ya raia wa Yemen wanaandamana katika mji wa bandari wa Aden kusini mwa nchi hiyo kutaka eneo hilo lijitenge kutoka kwa nchi hiyo. Waandamanaji mjini humo wanadai taifa la zamani la Yemen Kusini lilokuwa huru lirejeshwe.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Iddi Ssessanga