1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo Merkel-Brown

15 Januari 2009

Waziri mkuu Brown amtembelea Merkel Berlin

https://p.dw.com/p/GZ8c
Merkel na Brown.Picha: AP

Uingereza na Ujerumani, zilijaribu leo kutatua tofauti zao katika sera za uchumi huku waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown,akiipongeza mno Ujerumani kwa mradi wake ilioupitisha hivi punde kuutia jeki uchumi wake ulioanza kudoroa.

Katika mkutano wake na Kanzela Angela Merkel mjini Berlin leo na akiwa na shabaha ya kumaliza ugomvi wao ulioibuka mwishoni mwa mwaka jana ,waziri mkuu wa Uingereza alisemakuwa, Ujerumani punde hivi imepitisha mradi wa Euro bilłioni 50 kuufufua uchumi na huo -alisema-ni mfano mzuri kuigwa na nchi nyengine.

"Naamini uongozi uliochukuliwa na Ujerumani utakuwa mfano wa kufuatwa na wengine na umekuja wakati muafaka kuwa kuwa rais -mteule barack Obama anakaribia kushika madaraka." Alisema Bw.Brown baada ya mazungumzo yake na Kanzela angela Merkel.

Akaongeza na ninamnukulu,

"Watu wanahitaji msaada kweli tangu kwa familia zao hata kwa biashara zao na ndio maana hatua ilizoamua Ujerumani na Marekani nayo ikikaribia kuzipitisha,ni muhimu."

Angela Merkel hapo kabla alipagizwa jina "Bibi No"-mbishi na miji mingine ya Ulaya baada ya hatua za kwanza za kuufufua uchumi iliochukua ujerumani mwaka jana kuonekana hazitoshi kuuchangamsha uchumi unaoongoza barani ulaya .

Ubishi uliooneshwa na Ujerumani katika kukataa kuchukua hatua imara kukaonekana ndio sababu wakati ule Kanzela Merkel hakualikwa kuhudhuria kile kikao kilichofanyika London kati ya waziri mkuu Brown,rais Nicholai sarkozy wa Ufaransa na rais wa Tume ya Ulaya Jose Manuel Barroso mwezi uliopita.

Hii ikapelekea wakati ule waziri wa nje wa Ujerumani na naibu Kanzela Frank- walter Steinmeier, kulalamika aliposema,

"sidhani ni sawa kwa viongozi 3 kukutana bila kumualika Kanzela."

London na Brussels, zikachukua hatua kupooza mambo,lakini mvutano huo ukafufuka tena siku chache baadae pale waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrueck, alipovurumisha hujuma kali kupinga mkakati wa Uingereza wa kupunguza kodi ya (VAT) na kuongeza madeni.

Jaribio la pili la Ujerumani iliolopitisha juzi jumatatu kuzima kile inachohofia kuzorota vibaya kwa kwa uchumi wake tangu kupita miongo 6,linajumuisha kitita cha kati ya Euro bilioni 17-18 kujenga miundo-mbinu-barabara na mashule na Euro bilioni 9 kutumika kuwapunguzia wananchi na viwanda kodi.

Akiwajibu wakosoaji wake, kanzela Merkel alisema serikali yake ya muungano, ilifanya uchambuzi makini juu ya hali ya mambo na imeamua wakati umewadia sasa, kuchukua hatua za dharura ilizotangaza.