1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Makka

Oummilkheir6 Februari 2007

Rais Mahmoud Abbas wa Palastina na kiongozi wa Hamas anaeishi uhamishoni,Khaled Mechaal wanakutana hii leo mjini Makka kusaka makubaliano ambayo mfalme Abdallah wa Saud Arabia anasema yatawalazimisha wapalastina waache kuuwana.

https://p.dw.com/p/CHKf
Kitambulisho cha amani kati ya Israel na palastina
Kitambulisho cha amani kati ya Israel na palastinaPicha: AP Graphics/DW

Makubaliano ya mwisho ya kuweka chini silaha yaliyofikiwa ijumaa iliyopita yanaonyesha kuheshimiwa na Fatah na Hamas katika eneo la ukanda wa Gaza.

Wapalastina 66 wameuliw katika mapigano kati ya wanaharakati wa pande hizo mbili zinazohasimiana tangu january 25 iliyopita-mapambano makali kabisa kuwahi kushuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni huko Gaza,yakigubikwa na mzozo wa akisiasa na kifedha usiokua na kifani.

Katika mji mtukufu kwa waumini wa dini ya kiislam,Makka,ndiko Mahmoud Abbas na Khaled Mechaal wanakojaribu kusawazisha tofauti zao zinazokorofisha kuundwa serikali ya umoja wa taifa licha ya miezi kadhaa ya mazungumzo.

Mfalme Abdallah atakaekutana nao baadae hii leo,anataraji mazungumzo hayo yatapelekea kupatikana makubaliano yatakayoheshimiwa na pande hizo mbili.

“Nataraji ndugu hawa wataondoka katika maeneo matukufu kwa kufikia makubaliano ya dhati na watatambua umuhimu wa kusitisha umwagaji damu”amesema mfalme Abdallah aliyenukuliwa hii leo na shirika la habari la Suudia-SPA.

Waziri mkuu wa Palastina Ismael Haniyeh nae pia atashiriki mazungumzoni,katika wakati ambapo mazungumzo ya kunda serikali ya umoja wa taifa yanakwama katika masuala muhimu ya uhusiano pamoja na Israel na kugawana nyadhifa za serikali .

“Tunakwenda Makka tukiwa na matumaini mema ya kufikia makubaliano yatakayotuwezesha kuunusuru umoja wetu,kuupa nguvu ushirikiano wetu wa kisiasa na kuponya majaraha tulio nayo.”Amesema waziri mkuu Ismael Hanniyeh mbele ya waandishi habari kabla ya kuondoka Gaza kwenda Misri atakakoondokea kwenda Makka nchini Saud Arabia.

Bwana Hanniyeh ameahidi watafanya kila liwezekanalo kufikia makubaliano ya kuundwa serikali ya umoja.

“Bado kuna masuala kadhaa tete,lakini tunaahidi,tutafanya kila la kufanya kwa moyo mkunjufu ili kuyafumbua masuala yaliyosalia.” Mwisho wa kumnukuu kiongozi wa Hamas Ismael Hanniyeh.

Mkuu wa kundi la Fatah bungeni Azzam Al Ahmad anasema makubaliano yatabidi yaambatane na ratiba ya kisiasa ya chama chao.

“Serikali inabidi iheshimu ratiba hiyo pamoja na makubaliano yaliyofikiwa ili vizuwizi viweze kuondolewa”Amesema Azzam Al Ahmad alipokua akihojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Amani ya mashariki ya kati ni mada iliyogubika pia ziara inayomalizika hii lero ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika eneo hilo.