1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Amani ya Mashariki ya Kati Yakwama

9 Aprili 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema tangazo la Israel la ujenzi wa nyumba 700 katika eneo la mashariki la Jerusalem ndio chanzo cha kukurubia kuvunjika mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina

https://p.dw.com/p/1BeGs
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alipotuwa Tel Aviv 1.04.2014 katika juhudi za kuyafufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na palastinaPicha: Reuters

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani aliyekuwa akihojiwa na bunge la Marekani-Congress amesema pande zote mbili zimechukua hatua "zisizokuwa na maana"" na kwamba anataraji zitapata njia ya namna ya kurejea tena katika meza ya mazungumzo chini ya misingi madhubuti.

Wawakilishi wa Israel na Palastina katika meza ya mazungumzo wameagana, baada ya duru mpya ya mazungumzo iliyosimamiwa na Marekani,bila ya kupiga hatua yoyote mbele, katika juhudi za kuufufua utaratibu wa amani ya mashariki ya kati.

Miongoni mwa "hatua zisizokuwa na maana" zilizozusha pingamizi ni pamoja na kutoachiliwa huru kundi la nne na la mwisho la wafungwa wa kipalastina licha ya ahadi zilizotolewa,tangazo la ujenzi wa majumba 708 Jerusalem ya Mashariki-eneo ambalo wapalastina wanataka liwe mji mkuu wa taifa lao la siku za mbele pamoja na uamuzi wa wapalastina kutia saini wiki iliyopita makubaliano 15 ya kimataifa ikiwa ni pamoja na yale ya mjini Geneva kuhusu vita.

"Pande zote mbili,amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry mbele ya halmashauri ya baraza la Senet inayoshughulikia siasa ya nje,naiwe makusudi au bila ya kudhamiria,zimemalizikia kwa kupitisha mambo yasiyokuwa na maana."

John Kerry ameelezea matumaini yake kuona hata hivyo pande hizi mbili zinamlaani shetani na kurejea katika meza ya mazungumzo."Tunajaribu kuwatanabahisha lakini wao ndio wanaobidi kupitisha uamuzi wa kimsingi na nataraji watafanya hivyo hivyo" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.

China yaisihi Israel ipitishe hatua za kijasiri

Wakati huo huo rais Xi Jinping wa China ameitolea wito Israel ichukue "uamuzi jasiri" katika meza ya mazungumzo pamoja na wapalastina ."Utaratibu wa mazungumzo kati ya Israel na Palastina umeingia katika awamu muhimu-kuna fursa,sawa na mashaka yanayoweza kutokea" amesema rais Xi-Jinping wakati wa mazungumzo pamoja na rais Shimon Peres wa Israel mjini Beijing.

Shimon Peres Besuch in China mit Xi Jinping 08.04.2014
Rais wa Israel Shimon Perez (kulia) na mwenyeji wake,rais Xi Jinping wa China mjini BeijingPicha: Reuters

Nchini Israel kwenyewe waziri mkuu Benjamin NEtanyahu amewaamuru mawaziri wake wapunguze maingiliano yote isipokuwa ya kidiplomasia na usalama tu pamoja na wapalastina.Afisa mmoja wa Israel ambae hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP " hilo ni jibu kwa uamuzi wa Palastina wa kuvunja ahadi walizotoa kuelekea mazungumzo ya amani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu