1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria, je yapo matumaini?

John Juma
23 Februari 2017

Mazungumzo ya amani ya Syria yanaanza leo mjini Geneva, Switzerland huku kukiwa na shaka la uwezekano wa kupatikana kwa maelewano ya moja kwa moja.

https://p.dw.com/p/2Y7XP
Schweiz Syrien Friedensgespräche
Picha: picture alliance/dpa/F. Coffrini

Mazungumzo ya amani ya kutafuta suluhisho la kumaliza vita vya Syria yanaanza leo mjini Geneva, Switzerland. Hata hivyo Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Steffan de Mistura ametilia shaka uwezekano wa kupatikana kwa muafaka wa moja kwa moja. Swali kuu ni je yapo matumaini?

Kwa mara ya kwanza mazungumzo hayo yataongozwa na wapatanishi kutoka Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yanayoanza tena baada ya miezi kumi ya mkwamo tangu mazungumzo makuu ya awali kuvunjika Aprili 2016. Lakini kutokana na kutoaminiana, tofauti zilizopo pamoja na upinzani ambao umegawika, Mjumbe Maalum wa Umoja huo Steffan de Mistura ametilia shaka uwezekano wa kuafikia mapatano ya moja kwa moja lakini anatilia msisitizo umuhimu wa kuanza kwa mazungumzo yenyewe. "Je ninatumai kupata suluhisho? La hasha. Sitarajii mapatano ya moja kwa moja katika duru hii ya mazungumzo. Lakini ni mwanzo wa misururu ya mazungumzo ambayo yanapaswa kuwezesha masuala muhimu yanayohitajika kujadiliwa kwa kina ili kupata suluhisho la kisiasa."

Mkataba wa usitishwaji vita

Staffan de Mistura
Staffan de MisturaPicha: Reuters/D. Balibouse

Mkataba wa usitishwaji mapigano hukiukwa hali ambayo imechangia kuenea kwa uhasama. Steffan de Mistura ambaye ni mwanadiplomasia wa muda mrefu amesema kuwa ameiambia Urusi na Syria kusitisha mashambulio katika kipindi ambacho mazungumzo yanaendelea.

Hii ni awamu ya nne ambapo mazungumzo hayo yanafanywa Geneva. Katika awamu zote tatu zilizotangulia, hakujakuwepo mazungumzo ya uso kwa uso kati ya wawakilishi wa serikali na upinzani. Hata hivyo Steffan de Mistura ameelezea matumaini kuwa pande zote zitaketi kwenye meza moja wakati huu. Upande wa upinzani tayari umesema unataka mazungumzo ya ana kwa ana jinsi ilivyokuwa katika mazungumzo yaliyofanywa Astana, Kazakhstan wiki iliyopita, chini ya upatanisho wa Urusi na Uturuki. Hata hivyo mazungumzo hayo pia hayakufua dafu jinsi ilivyotarajiwa.

Mpiganaji wa FSA nchini Syria
Mpiganaji wa FSA nchini SyriaPicha: picture alliance/abaca/M. Nour

Salem al-Muslet amesema "Tunataka mazungumzo ya moja kwa moja, tunataka tuwe na mazungumzo ya kuonana. Hatutaki mazungumzo yafanyike kama awali kwenye vyumba ambapo hatujui nani yumo mle. Tunataka watu kujitolea kikamilifu kwenye meza ya mazungumzo, ndiyo sababu tunasisitiza mazungumzo ya ana kwa ana kupunguza wakati kwani kila siku inatugharimu nafsi zaidi, njaa na mashambulio kwetu na Wasyria"

Miongoni mwa masuala ambayo yanakusudiwa kujadiliwa ni pamoja na kuwepo kwa utawala wa mpito, kama suluhisho la kisiasa kumaliza mgogoro huo. Upinzani unahusisha suala hilo na wito wao wa kutaka rais Assad kuondoka madarakani. Hata hivyo upande wa serikali umeshikilia kuwa hatima ya rais haipaswi kujadiliwa.

Zaidi ya watu 300,000 wameuawa Syria na nusu ya watu wote nchini humo kupoteza makazi yao tangu vita hivyo vilivyoanza mwaka 2011, wakati ambapo vikosi vya serikali vilianzisha mashambulio dhidi ya waandamanaji waliomtaka Rais Assad kuacha mamlaka.

 

Mwandishi: John Juma /APE/RTRE

Mhariri: Gakuba Daniel