1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kudhibiti plastiki yakumbwa na kutoelewana

20 Novemba 2023

Duru ya tatu ya mazungumzo yanayolenga kuwasilisha mkataba wa kwanza duniani wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya plastiki, umetoa zaidi ya mapendekezo 500 kutoka serikali mbalimbali duniani.

https://p.dw.com/p/4Z9m7
Kenya | Maandamano juu ya uchafuzi wa plastiki
Wanaharakati wa mazingira wakiandamana kushinikiza kupunguzwa kwa matumizi ya plastikiPicha: Luis TatoAFP/Getty Images

Washiriki kwenye mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa, ambao walikutana katika mji mkuu wa Nairobi kwa mazungumzo ya wiki moja yanayojulikana kama INC3, wana hadi mwisho wa mwaka ujao kuja na mpango mahsusi wa kudhibiti plastiki, ambazo hukadiriwa kutoa tani milioni 400 za taka kila mwaka.

Wazalishaji wa plastiki na wauzaji wa mafuta ikiwemo Urusi na Saudi Arabia, wamesema makubaliano ya kimataifa yanapaswa kujikita katika kuchakata plastiki japo wanaharakati wa mazingira na baadhi ya serikali, wanapendekeza kuzalishwa kwa kiwango kidogo tu cha plastiki.

Kundi la mazingira la Greenpeace limeeleza kuwa, ili kuwepo kwa mpango wa pamoja utakaokuwa na mafanikio, basi Marekani na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuonyesha mfano mzuri zaidi wa uongozi tofauti na wanavyofanya sasa.Duru mbili zaidi za mazungumzo zitafanyika mwaka ujao ili kujaribu kuwasilisha mkataba wa kwanza duniani wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na matumizi ya plastiki.