1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuunda serikali yasita Sudan

Iddi Ssessanga
16 Mei 2019

Baraza la kijeshi nchini Sudan na makundi ya upinzani wamesitisha mashauriano kwa saa 72, muda mfupi baada ya kukubaliana kuhusu kipindi cha mpito cha miaka mitatu kuelekea kuundwa kwa serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3Iaf4
Sudan Protest
Picha: Getty Images/AFP/M. el-Shahed

Kiongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) Abdul Fattah al-Burhan kupitia kituo cha kitaifa cha runinga alisema kuwa mashauriano hayo yangeliahirishwa hadi waandamanaji watakapoondoa vizuizi vyote na kufungua barabara, vivukio vya bahari na reli zilizokuwa zimefungwa  katika mji mkuu, Khartoum.

Hatua hiyo ilikuja baada ya baraza hilo la kijeshi na waandamanaji kutangaza kuhusu muafaka katika mashauriano yao siku ya Jumatano (15 Mei).

Burhan aliongeza kuwa TMC iliamua kuondoa vizuizi vyote na kwamba vizuizi hivyo vinasababisha ghasia na kutatiza usalama.

Awali pande hizo mbili zilikuwa zimefikia makubaliano ya kugawanya madaraka ambapo kundi kuu la upinzani, Declaration of Freedom and Change Forces (DFCF) lingelipata thuluthi mbili za viti katika baraza hilo la  mpito la muda huku thuluthi moja iliyosalia ikiviendea vyama vingine vya kisiasa.

Upinzani wakosoa amri ya jeshi

Sudan Khartum Proteste am Militärhauptquartier
Waandamanaji wapinga hatua ya baraza la kijeshi kuahirisha mazungumzo ya kukabidhiana madaraka mjini Khartoum.Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Viongozi wa upinzani walikosoa hatua hiyo ya kusitisha mashauriano na wawakilishi wake kuhusu ubadilishanaji madaraka kwa njia ya amani kwa raia. Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamis (Mei 16), muungano huo wa wataalamu ulioongoza maandamno tangu mwezi Desemba ulisema kuwa hatua hiyo ni ya kusikitisha na haiheshimu hatua zilizopigwa wakati wa mashauriano hayo.

Hata hivyo,  baraza la TMC na kundi la DFCF bado hayakuwa yamekubaliana kuhusu kubuniwa kwa baraza huru ambalo ndilo chombo cha juu cha mamlaka litakaloongoza nchi hiyo hadi uchaguzi utakapofanyika .

Bado hakukuwa na makubaliano kuhusu kiwango ambacho jeshi na upande wa raia watapata katika baraza hilo.

Maandamano dhidi ya serikali yalianza nchini humo mwishoni mwa mwaka jana huku waandamanaji wakitoa wito kwa kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Omar al-Bashir kung'atuka madarakani.

Jeshi liliiingilia kati mnamo mwezi Aprili na kupanga mapinduzi na hatimaye kumkamata Bashir. Lakini waandamanaji wanasema kuwa viongozi wa kijeshi wanaendeleza utawala uliopita.

Tatu Karema/dpa