1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mzozo wa uchumi Ulaya

18 Septemba 2011

Mawaziri wa fedha wa nchi zinazoitumia sarafu ya euro wamekutana mjini Virostlav nchini Poland kwa mazungumzo ya siku mbili kuhusu mzozo wa madeni katika nchi zao

https://p.dw.com/p/12bOb
Ni majadiliano kuhusu sarafu ya euroPicha: dapd

Mawaziri hao wa fedha waliamua kuahirisha uamuzi kuhusu uwezekano wa mkopo wa pili kwa Ugiriki hadi mwezi Oktoba.

Griechenland George Papandreou
Waziri mkuu wa Ugiriki George PapandreouPicha: dapd

Rais wa kundi la mataifa hayo Jean Claude Juncker amesema Umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimatiafa IMF zinahitaji kuona mageuzi yakiendelezwa nchini Ugiriki kabla ya kutolewa awamu nyengine ya mkopo.


Wakati huo huo waziri wa fedha wa Marekani Timothy Geithner ambaye alihudhuria mazungumzo hayo, ameziomba nchi zinazotumia sarafu ya euro kuendeleza mipango itakayoinua uchumi wa nchi hizo badala ya kuangalia sana tatizo la matumizi ya serikali.

ECOFIN Treffen Breslau Timothy Geithner
Waziri wa fedha wa Marekani Timothy GeithnerPicha: dapd

Mawaziri walipinga vikali matamshi hayo na kuiambia Marekani kutatua matatizo yake. Nje ya mkutano huo, kiasi ya waandamanaji 40,000 wanaopinga hatua za kubana matumizi walikwamisha shughuli katika mji huo hapo jana.

Mazungumzo hayo yalilazimika kumalizika mapema kutokana na maandamano hayo.

Wakati huo huo waziri wa fedha wa Ujerumani kwa mara nyengine tena ametoa wito wa kutozwa kodi kwa biashara za fedha miongoni mwa nchi 17 zinazotumia sarafu ya euro.

Wolfgang Schäuble ameliambia gazeti la kila jumapili nchini Ujerumani la Bild am Sontag kuwa kodi hiyo itapangwa baadaye mwaka huu licha ya upinzani kutoka mataifa kama vile Marekani na Uingereza.

Deutschland Bundesfinanzminister Wolfgang Schäuble zu Urteil Bundesverfassungsgericht
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchaeublePicha: dapd

Waziri mwenzake wa Ubelgiji, Didier Reynders alimuunga mkono akisema kuwa kodi hiyo inahitajika kuyatuliza masoko.Waungaji mkono hatua hiyo kama vile Ujerumani, na Ufaransa zinaamini kuwa kodi hiyo itasitisha ulanguzi,na kusaidia kupatikana fedha zitakazoweza kutumika kutoa mikopo kwa mabenki katika wakati wa mizozo katika siku zinazokuja.

Wapinzani wanalalamika kuwa kodi ya aina hiyo itahamishia biashara kwenye masoko ya nchi ambazo hazitozi kodi.

Mwandishi Maryam Abdalla/all
Mhariri:Kitojo Sekione