1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Yemen yaendelea Geneva

Admin.WagnerD17 Juni 2015

Mazungumzo baina ya pande mbili zinazozozana Yemen yakiwa yanaendelea mashambulizi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia bado yauwa raia , huku tawi la al-Qaida nchini humo likiwauwa raia wawili wa Saudia

https://p.dw.com/p/1Fini
UN Genf Gespräche Jemen
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mazungumzo hayo baina ya serikali ya Yemen inayoendesha shughuli zake uhamishoni na wanamgambo wa Kihouthi yameingia siku yake ya tatu leo na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed, amesema katika hali kama hii ni vizuri pande zote mbili zinazozozana kuzungumza baina yao uso kwa uso bila ya kusimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa Mauritania amesisitiza kuwa licha ya mapungufu ya hapa na pale kwenye mazungumzo hayo, huu ni mwanzo mzuri.

Moja ya vikwazo vikubwa kwenye mazungumzo hayo ni misimamo inayong'ang'aniwa na kila upande. Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen, Riad Yassin, amesema msimamo wa serikali yake iliyoko uhamishoni Saudi Arabia haujabadilika na kwamba ni lazima waasi wa Kihouthi waondoke kwanza katika maeneo wanayoyadhibiti ndipo mashambulizi yatakapositishwa.

Naye kiongozi wa waasi hao, Abdulmalek al-Houthi, amesema serikali ya Yemen inajaribu kumtumia mjumbe wa Umoja wa Mataifa kulazimisha ajenda zao katika mazungumzo hayo.

Huku mazungumzo hayo yakiendelea, tawi la kundi la al-Qaida katika Ghuba ya Arabuni ambalo jana lilithibitisha kifo cha kiongozi wake, Nasir al-Wuhayshi, katika mashambulizi yaliyofanywa kusini mashariki mwa Yemen wiki iliyopita, limetangaza leo kuwa limewauwa raia wawili wa Saudi Arabia kwa kile lilichodai ni kuhusika kwao na mauaji hayo ya kiongozi wao.

Jemen Al-Qaida Nasser al-Wahischi
Kiongozi wa tawi la al-Qaeda la Yemen Nasir al-WuhayshiPicha: AFP/GettyImages

Marekani imesema kifo cha kiongozi huyo ni pigo kubwa kwa kundi hilo. Mashahidi wanasema miili ya Wasaudia hao wawili ilitundikwa katika daraja, ikiwa ni adhabu ya kuifanyia ujasusi Marekani.

Kwa upande mwengine, vyombo vya habari nchini Yemen vimeripoti hii leo kufanyika kwa mashambulizi ya anga ya mataifa ya Kiarabu yakiongozwa na Saudi Arabia, ambapo idadi ya watu waliokufa kwenye mashambulizi hayo imepindukia 30. Kwa mujibu wa mashahidi, ndege hizo za kijeshi ziliushambulia msafara wa raia waliokuwa wakikimbia maeneo yaliyokumbwa na vita katika mji wa Aden, kusini mwa Yemen.

Saudi Arabia bado haijasema lolote kuhusiana na mashambulizi hayo, ambayo kama yatathibitishwa basi ni doa jengine kwenye kampeni yake dhidi ya waasi wa Kihouthi.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha mzozo huo unaoendelea nchini Yemen tayari umeshauwa takriban watu 1,400 hadi sasa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef