1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinyo waongezeka dhidi ya mahasimu Sudan kusini

29 Desemba 2013

Mbinyo wa kimataifa unaongezeka dhidi ya pande mbili nchini Sudan kusini kuanza mazungumzo ya amani, ili kuzuwia taifa hilo changa kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/1Ai5n
IGAD Treffen Nairobi
Viongozi wa IGAD katika mkutano mjini NairobiPicha: picture-alliance/dpa

Wapatanishi wa amani kutoka mataifa ya Afrika mashariki na pembe ya Afrika wametoa hadi Desemba 31 kwa rais Salva Kiir na kiongozi rasmi wa waasi hivi sasa Riek Machar, ambaye kiir alimfuta kazi kama makamu wake wa rais Julai mwaka huu, kuanza mazungumzo ya ana kwa ana na kusitisha mapigano ya wiki mbili ambayo yanafikiriwa kuwa yamesababisha watu zaidi ya elfu moja kuuwawa.

"Upande wa serikali, tuko tayari kukutana hata kabla ya hapo," makamu wa rais wa Sudan kusini James Wani Igga amewaambia waandishi habari. "sasa ni juu ya Machar kukubali kusitisha mapigano."

Äthiopiens Premierminister Hailemariam Desalegn, Südsudan Salva Kiir und Präsident Kenias Präsident Uhuru Kenyatta
Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn,Salva Kiir wa Sudan kusini na Uhuru Kenyatta wa KenyaPicha: picture-alliance/dpa

Serikali siku ya Jumamosi imerudia shutuma zake kuwa Machar anawakusanya maelfu ya vijana kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na serikali hiyo.

Shutuma dhidi ya Machar

"Dr. Riek Machar anawakusanya vijana , kiasi ya 25,000, na anataka kuwatumia kushambulia serikali" katika jimbo la mashariki la Jonglei, ambako waasi ambao wanaelezwa kuwa wanamuunga mkono Machar walikamata kwa muda mji mkuu wa jimbo hilo, la Bor, mapema mwezi huu, amesema msemaji wa serikali Michael Makuei katika mahojiano na shirika la habari la AFP.

"Wana uwezo wa kushambulia wakati wowote," ameongeza. "Tuko katika hali ya tahadhari kuwalinda raia."

Präsident Salva Kiir Südsudan Süd Sudan Porträt
Salva KiirPicha: Reuters

Lakini Moses Ruai Lat, msemaji wa waasi, amelikataa hilo, akisema makamu wa rais wa zamani , "hajawakusanya watu wa kabila lake," la Nuer , ikiwa ni kabila la pili kwa ukubwa katika Sudan kusini.

Vijana hao ni wanajeshi wa kawaida ambao wanakimbia kutoka jeshi la serikali na hawajaandikishwa na Machar, ameongeza.

Südsudan Riek Machar Vize-Präsident
Riek MacharPicha: Reuters

Kundi la eneo hilo la mamlaka ya maingiliano ya serikali kwa ajili ya maendeleo IGAD, linaongoza juhudi za kumaliza mapambano makali ya udhibiti ya maeneo kadha muhimu yanayotoa mafuta hususan katika eneo la kaskazini ya Sudan kusini.

Mbinyo waongezeka

Umoja wa mataifa , Marekani na China pia zinataka kufanyike mazungumzo. IGAD tayari imeweka masharti kwamba pande hizo mbili zinazopingana zinapaswa kujadiliana katika muda wa siku nne kuazia Ijumaa, " msemaji wa wiazara ya mambo ya kigeni ya Ethiopia Dina Mufti amesema jana Jumamosi, (28.12.2013).

Kiongozi wa waasi amesema kuwa kwanza anataka utaratibu wa kusimamia usitishaji wa mapigano pamoja na kuachiliwa huru kwa washirika wake wa kisiasa waliokamatwa wakati machafuko hayo yalipoanza.

Südsudan Flüchtlinge 18.12.2013
Wakimbizi wa ndani nchini Sudan kusini 18.12.2013Picha: picture-alliance/dpa

Mzozo huo uliochochewa na uhasama wa siku nyingi kati ya Kiir na Machar, umezidisha tofauti kati ya kabila la Kiir la Dinka na lile la Machar la Nuer katika nchi hiyo, ambayo ilijipatia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011.

Ripoti za mauaji, na ubakaji zimejitokeza hivi karibuni. Umoja wa Mataifa, ambayo walinzi wake wa amani ambao wamebeba mzigo mkubwa wanaongezwa hadi wanajeshi 12,000, umesema kaburi moja lililozikwa watu wengi limegunduliwa na idadi kubwa ya miili ambayo bado haijaondolewa imeonekana nje ya takriban kituo kimoja cha Umoja huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Sudi Mnette