1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge wa AfD apigwa vibaya sana Bremen

Oumilkheir Hamidou
8 Januari 2019

Viongozi wa vyama vyote vya kisiasa nchini Ujerumani wamelaani shambulio la kikatili dhidi ya mbunge na kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia katika jimbo la Bremen, Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD.

https://p.dw.com/p/3BCEL
Berlin: Frank Magnitz (AfD), Bundestagsabgeordneter
Picha: picture-alliance/dpa/F. Sommer

"Shambulio hilo la kikatili linabidi lilaaniwe kwa nguvu.Tutaraji polisi watafanikiwa kuwakamata haraka wahalifu" amesema msemaji wa kansela Angela Merkel na serikali kuu ya Ujerumani, Steffen Seibert kupitia mtandao wa Twitter.

Kwa mujibu wa polisi, shambulio dhidi ya Frank Magnitz, mwenye umri wa miaka 66 ,mbunge wa shirikisho na kiongozi wa tawi la chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD katika jimbo la kaskazini la Bremen limetokea jana jioni kati kati ya mji wa Bremen.

Chama cha AfD kimechapisha kwa upande wake picha ya mbunge huyo akiwa amelazwa hospitalini, uso ukiwa umejaa damu.

Polisi wanachunguza kisa cha kupigwa mwanasiasa wa AfD mjini Bremen
Polisi wanachunguza kisa cha kupigwa mwanasiasa wa AfD mjini BremenPicha: Reuters/F. Bimmer

"Wametaka kumuuwa makusudi", wanasema AfD

Katika taarifa yake polisi wanasema Frank Magnitz ameshambuliwa na watu watatu walioficha nyuso zao."Wamempiga virungu kichwani mpaka akazimia na baadae kumpiga mateke" -ripoti ya AfD imesema.

"Walitaka kumuuwa", mwenyekiti wa chama hicho Alexander Gauland amesema na kutuhumu siasa iko nyuma ya shambulio hilo. Gauland amewalaumu wanasiasa anaodai wamejitenga na chama cha AfD na kupania kuwazuwia wasitwae madaraka.

"Ni sehemu ya mbinu ya kutaka kututenga na kukihujumu chama cha AfD" amesema Gauland aliyezungumzia juhudi za kukipeleleza chama chao pamoja na mbinu za kutaka kukizuwia chama hicho kisiwe naibu spika wa bunge la shirikisho Bundestag.

Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer akizungumzia kadhia ya udukuzi
Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer akizungumzia kadhia ya udukuziPicha: Reuters/F. Bensch

Mdukuzi atiwa mbaroni

Wakati huo huo, kijana wa miaka 20, mwanafunzi ambae mpaka sasa anaishi na wazazi wake amekamatwa kuhusika na kisa cha kudukua data za mamia ya wanasiasa wa vyama vyote isipokuwa wale wa AfD, waandishi habari, wasanii na watu wengine kadhaa mashuhuri.

Msemaji wa idara inayopambana na uhalifu wa mtandaoni katika ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu mjini Frankfurt, Georg Ungefuk, amesema hakuna dalili yoyote kwa sasa kama kijana huyo ana mafungamano na siasa kali za mrengo wa kulia."Mdukuzi amejipatia maarifa ya kiufundi kutokana na kupitisha muda mrefu katika komputa-amesema Ungefuk.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AP

Mhariri: Caro Robi