1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa Trump waonyeshwa kwenye runinga

14 Novemba 2019

Mchakato wa uchunguzi wa kutaka kumshitaki Rais wa Marekani Donald Trump wa Marekani umeanza kupeperushwa mubashara kwa njia ya televisheni kwa mara ya kwanza hapo jana.

https://p.dw.com/p/3T3Fn
US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/abaca/Y. Gripas

Wanadiplomasia William Tailor na George Kent wametoa ushahidi wao mbele ya  kamati ya baraza la mawakili katika awamu ya kwanza ya mchakato huo ambao unaweka wadhifa na uchaguzi wa muhula wa pili wa rais Trump katika wasiwasi.

Wanadiplomasia hao wametoa ushahidi kuwa walipokea shinikizo kutoka kwa rais Trump na washirika wake kuibana Ukraine kumfanyia uchunguzi hasimu wake wa kisisia makamu wa rais wa zamani, Joe Biden na mwanawe katika biashara zao nchini Ukraine.

Walitoa ushahidi wao wakiwa watulivu lakini haikuwa wazi ikiwa ushahidi huo utakisaidia  chama cha Democratic kuondoa mpasuko na tofauti zilizopo na kuwashawishi Wamarekani zaidi kwamba rais wa chama cha Republican alifanya makosa mabaya yanayostahili kumuondoa ofisini.

Taylor asema alisikia mazungumzo ya Trump

Katika ushahidi wale Taylor alisema mmoja wa wafanyikazi wake alisikia mazungumzo ya simu ya Julai 26, simu kati ya Trump na Gordon Sondland, mshirika wa zamani wa kisiasa wa rais Trump na alisikika akiulizia kuhusu uchunguzi huo na Sondland alimwambia Trump Ukraine walikuwa tayari kuendelea.

Tailor katika ushahidi wake alisema, "Wakati wa mawasiliano yangu ya baadaye na Balozi Volker na Sondland wananiambia kwamba rais alitaka kusikia kutoka Zelinskiy kabla ya kupanga mkutano katika Ofisi ya rais. Haikuwa wazi kwangu hii inamaanisha nini. Mnamo Juni 27 Balozi Sondland aliniambia wakati wa mazungumzo ya simu kwamba Rais Zelinskiy alihitaji kuweka wazi kwa Rais Trump kwamba yeye na Rais Zelinskiy hawakuwa wanazuia uchunguzi."

Kwa upande wake George Kent alisema, "Kama kiongozi, siamini kuwa Marekani inapaswa kuiomba nchi nyengine kufanya upelelezi wa upendeleo wa kisiasa au mashtaka dhidi ya wapinzani wa wale walioko madarakani, kwa sababu hatua hizo za kuchagua zinadhoofisha utawala wa sheria bila kujali nchi."

Uchunguzi huo unaoendelea kupeperushwa moja kwa moja kwenye televisheni umewavutia mamilioni ya watu. Mashahidi wengine waliopangwa kutoa ushidi wao wiki hii wanatarajiwa kusema wametiwa wasiwasi sana na hatua ya Trump kuomba msaada wa Ukraine kuwachunguza wanachama wa chama cha Democratic huku Marekani ikisitisha msaada wa kijeshi.

(ape, reuters)