1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mdahalo kuhusu usafi wa hospitali waibuka Ujerumani

25 Agosti 2010

Vifo vya watoto wachanga watatu vilivyotokea katika hospitali ya chuo kikuu mjini Mainz,vimezusha mdahalo mpya kuhusu usafi katika hospitali za Ujerumani.

https://p.dw.com/p/OvV3
Das Zentrum fuer Kinder- und Jugendmedizin der Universitaetsklinik Mainz, aufgenommen am Sonntag, 22. August 2010. (apn Photo/Kristina Schaefer)
Idara ya watoto na vijana katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Mainz.Picha: AP

Vipi jambo kama hilo limeweza kutokea? Hatua gani zinazoweza kuchukuliwa kuzuia jambo kama hilo kutokea tena? Hayo ni baadhi ya masuala yaliyozuka kufuatia vifo hivyo.

Mjini Mainz, watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au walio na matatizo ya moyo hupelekwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi kinachohudumia watoto na vijana katika hospitali ya chuo kikuu. Watoto hao wachanga hupewa mchanganyiko maalum wa chakula na dawa kwa njia ya mpira.Mchanganyiko huo hutayarishwa kila siku na wafanyakazi wawili katika maabara ya hospitali ndani ya chumba kilichokuwa na hewa safi.Hiyo ni kazi yao ya kawaida inayofanywa wakiwa na mavazi safi kabisa na hubadili glovu baada ya kila nusu saa. Kazi zote hufanywa kwa mashine isipokuwa mpira ndio hupachikwa kwa mkono. Baadae mchanganyiko huo huchunguzwa na taasisi ya mikrobiolojia katika hospitali hiyo ili kuhakikisha kuwa hakuna vijidudu vilivyoingia ndani. Lakini tatizo ni kuwa vijidudu vinaweza kuonekana baada ya saa ishirini na sio kabla.

Kwa hivyo, katika hospitali hiyo ya Mainz, watoto walipewa mchanganyiko huo wa chakula usiku mzima lakini hali yao iligeuka kuwa mbaya zaidi, na wawili walifariki asubuhi yake .Hiyo ilikuwa jumamosi iliyopita na mtoto wa tatu alifariki siku ya jumatatu. Ikagunduliwa kuwa chakula chao kilikuwa na vijidudu vya bakteria Enterobacter cloacae. Kuna aina 14 mbali mbali ya bakteria hiyo na kawaida hukutikana katika utumbo wa binadamu na aina fulani husaidia kusaga chakula. Lakini Eneterobacter ni bakteria ambayo mara nyingi ni vigumu kutibiwa kwa dawa za kupambana na bakteria na wagonjwa huambikzwa hospitali, hasa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Kufuatia vifo vya watoto hao watatu, hospitali za Ujerumani zimehimizwa kuimarisha ukaguzi wa usafi. Hivi sasa kazi hiyo husimamiwa na serikali za majimbo.Kutoka jumla ya majimbo 16, matatu tu ndio yaliyo na utaratibu maalum kuhusu usafi wa hospitali. Majimbo hayo ni Berlin, North Rhine Westphalia na Saarland.Tangu muda mrefu jumuiya ya usafi wa hospitali nchini Ujerumani imetaka iwepo sheria ya aina moja kusimamia usafi katika hospitali. Kwa mujibu wa msemaji wa jumuiya hiyo Klaus-Dieter Zastrow,kila mwaka nchini Ujerumani hadi watu milioni moja hupata maambukizo kadhaa wanapolazwa hospitali na kama watu 40,000 hufariki. Nusu ya vifo hivyo vingeweza kuepukwa kwa kufuata kikamilifu taratibu za usafi.

Der Bundesgesundheitsminister Philipp Rösler (FDP) hält am Mittwoch (10.03.2010) im Berliner Olympiastadion aus Anlass des bundesweiten Innovations- Wettbewerbs «Jugend denkt Zukunft" eine Rede. Foto: Alina Novopashina dpa/lbn
Waziri wa Afya wa Ujerumani, Philipp Rösler.Picha: picture-alliance/dpa

Sasa waziri wa afya wa Ujerumani Philipp Rösler anataka kuimarisha usafi wa hospitali kisheria.Lakini jumuiya ya madaktari wa Ujerumani inapinga kuziwekea hospitali kanuni mpya za usafi. Msemaji wao Hans-Jörg Freese amesema, hakuna uhaba wa miongozo - na sheria mpya wala haitosaidia kupambana na tatizo la usafi. Anaetaka udhibiti bora wa usafi aajiri wafanyakazi zaidi hospitalini. Lakini ni bora zaidi kwa kila hospitali kuwa na mjumbe maalum atakaesimamia usafi tu. Anasema,gharama hizo mpya lakini zisiathiri idara zingine. Bila shaka huu ni mwanzo tu wa majadiliano hayo.

Mwandishi: Nicklis,Petra/ZPR

Mhariri: Abdul-Rahman