1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mebazaa 'ayavulia kofia' mapinduzi

20 Januari 2011

Rais wa mpito wa Tunisia, Foued Mebazaa, ameahidi kuachana na mambo yaliyofanyika katika utawala uliopita na kupongeza mapinduzi ya heshima na uhuru. huku uchunguzi dhidi ya Zine El Abidine Ben Ali ukianzishwa rasmi.

https://p.dw.com/p/1002O
Rais wa muda wa Tunisia, Fouad Mebazaa
Rais wa muda wa Tunisia, Fouad MebazaaPicha: picture alliance/dpa

Rais Foued Mebazaa amesema kuwa wachunguzi watapeleleza kwa kina mali za ndani na nje ya nchi za kiongozi wa zamani wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali, aliyeondolewa madarakani na kukimbilia Saudi Arabia Ijumaa iliyopita. Akilihutubia taifa hapo jana, Rais Mebazaa alisema kwa pamoja wanaweza kufungua ukurasa mpya katika historia ya Tunisia.

Kiongozi huyo mpya ameahidi pia kuhakikisha anatoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa, kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa mahakama.Kituo cha televisheni ya taifa, kimeripoti kuwa ndugu 33 wa familia ya Ben Ali wamekamatwa kwa kile serikali ilichokiita, uhalifu dhidi ya taifa. Serikali hiyo imesema mali za Ben Ali zilizoko Tunisia, zimezuiliwa, huku Uswisi nayo ikisema imezuia akaunti za benki.

Baraza la Mawaziri lakutana

Waziri Mkuu wa Tunisia, Muhammad Ghannouchi (kushoto) na Rais Mebazaa
Waziri Mkuu wa Tunisia, Muhammad Ghannouchi (kushoto) na Rais MebazaaPicha: picture alliance / dpa

Wakati huo huo, mkutano wa kwanza wa baraza jipya la mawaziri nchini Tunisia unatarajiwa kufanyika leo, wakati ambapo maandamano mapya ya kupinga kubakishwa madarakani mawaziri waliokuwepo katika utawala uliopita wa Ben Ali na kuvunjwa kabisa chama tawala cha RCD, yakiendelea. Waandamanaji hao wamesema wanataka bunge jipya, katiba mpya na jamhuri mpya.

Marekani imeitaka serikali hiyo ya mpito kuelekea katika demokrasia ya kweli na imeahidi kutoa msaada wake. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Philip J.Crowley amesema kuwa wananchi wa Tunisia wamezungumza, hivyo serikali mpya haina budi kujenga demokrasia ya kweli. Akizungumza na wananchi kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Jumamosi iliyopita, Rais Mebazaa alilishukuru jeshi kwa kuhakikisha usalama wakati wa ghasia za hivi karibuni.

Hata hivyo, mazungumzo kuhusu kukijumuisha chama kikuu cha wafanyakazi cha UGTT katika serikali mpya, yalivunjika jana, kutokana na kujiuzulu kwa mawaziri wanne siku ya Jumanne. Serikali ilitoa vibali halali kwa vyama vitatu ambavyo vilizuiwa na utawala uliopita na kumwaachia mwandishi habari ambaye ni mpinzani, Fahem Boukadous, ambaye mwaka uliopita alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kutokana na kazi yake.

Kwa upande mwingine, mkosaiji mkubwa wa Ben Ali, mwanasiasa wa upinzani, Moncef Marzouki ambaye alitangaza nia ya kugombea katika uchaguzi wa rais, jana amerejea nchini Tunisia, baada ya kuishi uhamishoni Ufaransa kwa miaka kadhaa.

Naye mmoja kati ya wapinzani wakubwa wa Tunisia, Taoufik Ben Brik ametangaza kugombea katika uchaguzi ambao serikali ya mpito umeahidi utakuwa huru na wa haki. Aidha, Umoja wa Mataifa umesema unajiandaa kupeleka waangalizi wa haki za binaadamu nchini Tunisia wiki ijayo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani