1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mediterania Bahari ya kifo

Saumu Mwasimba
25 Novemba 2017

Bahari ya Mediterania ni njia hatari zaidi duniani kwa wahamiaji wanaofanya juhudi za kufika barani Ulaya-lasema shirika la uhamiaji la UN

https://p.dw.com/p/2oFSd
Italien Flüchtlinge werden von Hilfsorganisation Sea-Eye gerettet
Picha: picture alliance/dpa/NurPhoto/C. Marquardt

Zaidi ya watu 33,000 wamefariki wakijaribu kufanikisha safari hatari kabisa ya kuvuka bahari ya Meditterania  tangu mwaka 2000 kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa.Wakati njia kati ya  Uturuki na Ulaya ikiwa imefungwa shinikizo linazidi kuongezeka katika njia nyingine ya kuelekea Itali.Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limesema Ijumaa kwamba bahari ya Meditterania imebakia kuwa ndio kivuko hatari kabisa kinachoangamiza uhai wa watu wengi duniani huku  zaidi ya wakimbizi 33,000 wakifariki wakijaribu kuvuka kwa njia hatari kupitia bahari hiyo tangu mwaka 2000.

Hatari yaongezeka

Ijapokuwa idadi ya vifo imepungua tangu iliposhuhudiwa rekodi kubwa ya watu wanaowasili katika ardhi ya Ulaya tangu mwaka 2014 hadi 2016,hatari au kitisho cha kutokea vifo wakati wa safari hiyo kimeongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa na shirika la IOM.

Italien - Flüchtlingsboote - Mittelmeer
Picha: Getty Images/C. McGrath

Makubaliana yenye utata kuhusu suala la wakimbikizi yaliyofikiwa kati ya Uturuki pamoja na  vizuizi vya wanajeshi wa majini vilivyowekwa na jeshi la ulinzi wa pwani la Libya,vimeifanya safari ya kuvuka bahari ya Mediterania kuwa hatari zaidi kwasababu imewafanya watu kubadili njia na kutumia njia nyingine ndefu ya kuelekea Itali anasema Phillipe Fargues mmoja wa watu walioandika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa na pia ni profesa katika chuo kikuu cha Ulaya mjini Florence nchini Itali.

Mtaalamu huyo anasema kuifunga njia fupi iliyokuwa ikitumiwa mwanzo na wahamiaji ambayo sio hatari sana ni hatua inayoweza kufungua njia nyingine ndefu na zilizo hatari zaidi na hivyo basi kuongeza uwezekano wa watu wengi kupoteza maisha baharini.

Kadhalika anasema ushirikiano kati ya Ulaya na Uturuki wa kuzuia wimbi la wakimbizi sasa unafinikwa na Libya ambayo ni kituo kikuu hivi sasa cha wahamiaji wanaosubiri kuvukishwa kwa njia za magendo kuingia Ulaya.Hata hivyo mwelekeo huo sio tu haufai lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa kutofanikiwa kwa kuangalia ule ukweli kwamba Libya inakabiliwa na utawala mbaya ,ukosefu wa usalama na mgawanyiko wa kisiasa.

Wakimbizi wa kiuchumi waongezeka

Italien Flüchtlinge in Kalabrien | Sant' Alessio
Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Zaidi ya wahamiaji 161 na wakimbizi wamewasaili Ulaya mwaka huu  huku asilimia 75 ya wakimbizi hao wakiwasili Itali kupitia njia ya kati ya bahari ya Mediterania.Mwaka 2015 Umoja wa Ulaya ulishuhudia ongezeko kubwa kabisa la wahamiaji katika nchi hizo wengi wao wakiwa wamekimbia vita mashariki ya Kati,Asia na Afrika ambapo Ujerumani ilipokea  kiasi watu 900,000.

Hata hivyo serikali zinasema kwamba chini ya thuluthi moja ya wahamiaji waliowasili Itali  mwaka huu wanatafuta hifadhi ikitajwa kwamba ni wakimbizi wa kiuchumi.Wengi walioingia Ulaya mwaka huu wametokea Nigeria,Eritrea na Guinea.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Isaac Gamba

Source:DW ENG