1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel abatilisha mpango wa kufunga maduka wakati wa Pasaka

John Juma Mhariri: Daniel Gakuba
24 Machi 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amebatilisha mpango wa kuweka vizuizi vikali vya kudhibiti janga la virusi vya corona katika kipindi cha Pasaka baada ya ukosoaji mkubwa.

https://p.dw.com/p/3r47a
Berlin Kanzlerin Merkel vor Kabinettssitzung
Picha: picture alliance/dpa/dpa-Pool

Kansela Merkel na wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani walikubaliana baada ya mazungumzo ya saa nyingi ya Jumatatu kwamba maduka yote yalipaswa kufungwa kuanzia Aprili mosi hadi Aprili 5, na kuruhusu maduka ya vyakula tu kufunguliwa tarehe 3.

Lakini sasa wamefuta mpango huo. Badala yake, wamewahimiza raia kusalia majumbani katika kipindi cha Pasaka.

Mkuu wa chama cha Christian Democratic Union-CDU ambaye pia ni kiongozi wa jimbo la North Rhine-Westphalia  Armin Laschet ameliarifu bunge la jimbo hilo mjini Duesseldorf kuhusu mabadiliko hayo.

Soma pia:Waziri wa afya wa Ujerumani kuchunguzwa kashfa ya barakoa

Armin Laschet ameliambia bunge hilo kuwa hatua hiyo ilikuwa kosa na isingeweza kutekelezeka kwa namna ilivyo.

Kansela Angela Merkel akijibu maswali kutoka kwa wabunge katika bunge la Ujerumani Berlin 24.03.2021
Kansela Angela Merkel akijibu maswali kutoka kwa wabunge katika bunge la Ujerumani Berlin 24.03.2021Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Mapema leo, Kansela Angela Merkel aliitisha kikao cha dharura, kufuatia ukosoaji mkubwa wa umma dhidi ya hatua za kupambana na janga la COVID-19 ambazo pia zimesababisha viwango vya uungwaji mkono wa chama chake CDU kushuka. Kabla ya mkutano wake pia na waandishi wa habari, jarida la Der Spiegel liliripoti kwamba Angela Merkel mwenyewe pia alikiri kuwa mpango wa kuweka vizuizi vikali kipindi cha Pasaka ulikuwa kosa.

Merkel akiri mpango huo ulikowa kosa lake

Mkuu wa CDU, Armin Laschet amesema kwenye kikao hicho kuwa viongozi walitarajiwa kutathmini kwa undani nini ilifanyika siku mbili zilizopita.

Soma pia: Wabunge Ujerumani wajiuzulu baada ya kashfa ya barakoa

Daniel Guenther, ambaye ni mkuu wa jimbo la Schleswig-Holstein ameliambia shirika la habari la DPA kwamba kikao chao cha dharura kitajikita katika kile alichokitaja kuwa ‘utekelezaji wa makosa‘ kuhusiana na hatua zilizokubaliwa wakati wa Pasaka.

Wakoasoaji waikosoa serikali ya Ujerumani kuhusu namna inavyoshughulikia janga la COVID-19.
Wakoasoaji waikosoa serikali ya Ujerumani kuhusu namna inavyoshughulikia janga la COVID-19.Picha: Sina Schuldt/dpa/picture alliance

Serikali Ujerumani yakosolewa vikali

Hatua hizo zilizusha ukosoaji mkali, huku gazeti la kila siku la The Bild likitaja juhudi za serikali kushughulikia janga la COVID-19 kuwa "fujo", likiongeza kuwa Merkel pamoja na wakuu wa majimbo wamekosa kuona shida kamili.

Nalo jarida la Der Spiegel liliitaja hatua hiyo kuwa "kashfa”, likidai serikali imekosa kabisa kuhusu vipaumbele vyake na badala yake inapaswa kulenga kuimarisha kampeni ya utoaji chanjo na mkakati wa kupima maambukizo.

Idadi ya maambukizo ya virusi vya corona nchini Ujerumani imekuwa ikiongezeka. Katika muda wa saa 24 zilizopita, jumla ya watu 15,813 wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo, kulingana na taasisi ya Ujerumani inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza Robert Koch.