1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ahofia Trump anavyoivuruga Trans-Atlantiki

Mohammed Khelef
20 Julai 2018

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema licha ya mahusiano ya Ulaya na Marekani kupitia kipindi kigumu katika wakati huu chini ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, lakini bado ni muhimu sana kwa serikali yake.

https://p.dw.com/p/31pOn
Germany Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Kansela Merkel alisema kuwa hana uhakika ikiwa Ulaya itaweza haraka kuwa na uwezo wa kuzikabili changamoto za jukumu la kutatua migogoro ya dunia ya karne ya 21, katika wakati ambapo utawala wa Trump nchini Marekani unaonekana kujitenga kando  na wajibu huo.

Katika mkutano wake huo wa majira ya kiangazi na waandishi wa habari, Kansela Merkel alitumia muda mrefu kuzungumzia mahusiano ya Bahari ya Atlantiki, ambayo yanazileta pamoja Ulaya na Marekani, akisema kuwa bado yanasalia kuwa jambo muhimu kabisa kwenye serikali yake, licha ya wasiwasi uliopo kumuhusu Rais Trump. 

Mara kadhaa, Trump amekuwa akiikosoa Ujerumani kwa kile anachoona kuwa ni matumizi madogo sana ya kijeshi na pia mradi wa bomba la gesi linazoziunganisha Ujerumani na Urusi.

Mbele ya waandishi hao, Merkel alikiri kuwa utaratibu wa kimahusiano baina ya pande hizi mbili umejikuta kwenye wakati mgumu sana mbele ya utawala wa Marekani chini ya Trump. "Nadhani tunaweza kusema kwamba utaratibu tuliokuwa tumeuzowea unakabiliwa na shinikizo kubwa kwa sasa. Hata hivyo, mahusiano ya Bahari ya Atlantiki, yakiwemo yale na Rais wa Marekani, hapana shaka ni muhimu kwetu na nitaendelea kuyaengaenga."

Ulaya haimini kwenye nguvu za kijeshi pekee

Kansela huyo alisema licha ya kutambua shinikizo la Marekani la kutaka Ujerumani ibebe jukumu la kutatuwa migogoro duniani, kwake utatuzi huo haumaanishi pekee hatua za kijeshi, bali zaidi hatua za kisiasa, akipigia mfano ushiriki wa Ulaya kwenye migogoro barani Afrika, ambako Jumuiya ya Kujihami ya NATO haikuwako.

Sommerpressekonferenz Merkel
Mkutano wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waandishi wa habari kwenye majira ya kiangazi.Picha: Reuters/F. Bensch

Alihoji kwamba kwa sasa Umoja wa Ulaya upo kwenye kipindi cha mageuzi makubwa, na japokuwa inatambuwa uzito wa masuala ya kilimwengu yaliyopo, bado haijachukuwa uamuzi wa ikiwa ijiingize kwenye masuala hayo moja kwa moja kama yafanyavyo mataifa mengine makubwa duniani.

Pamoja na hayo, Merkel alisema, Ujerumani inapendelea sana ushirikiano wa mataifa mengi kwa pamoja kwenye utendaji mambo yake. "Kilicho muhimu kwangu, ambacho kimekuwa muhimu kwenye maisha yangu yote kisiasa ni ushirikiano wa mataifa mbalimbali, imani madhubuti kwamba ikiwa tutashirikiana, tunaweza kuwa na hali ambapo kila upande ni mshindi, yaani kuunda fursa za wote kunufaika. Hii hata kama sio kanuni inayotawala kwa sasa, hilo halitanivunja moyo na kunifanya nisiipiganie. Nadhani ndio njia pekee ya kuweza kusonga mbele."

Kuhusiana na mkutano wa hivi karibuni kati ya Trump na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, Kansela Merkel alisema mikutano ya aina hii inapaswa kuwa jambo la kawaida na kwamba ni vyema kwamba wawili hao wamekutana. 

Tayari Trump alitangaza kuwa atamkaribisha Putin mjini Washington baadaye mwaka huu, baada ya mkutano huo wa kwanza mjini Helsinki, Finland, Jumatatu iliyopita, ambao umemsababishia ukosowaji mkubwa kutoka ndani na nje ya chama chake cha Republican kwa kile wanachosema "aliidhalilisha Marekani mbele ya taifa hasimu."

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga