1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel alaani mashambulizi ya Munich

23 Julai 2016

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Wajerumani wanaomboleza watu waliokufa katika shambulizi la mjini Munich hapo jana na wanashirikiana na machungu ya familia na marafiki wa wahanga.

https://p.dw.com/p/1JUp2
Nach Schießerei in München Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Bi Merkel alikuwa akitoa kauli yake ya kwanza kuhusu mashambulizi hayo ya Ijumaa, ambapo watu tisa walipigwa risasi na kuuliwa na mshambuliaji kijana raia wa Ujerumani wa umri ya miaka 18 mwenye asili ya Iran, kabla kujiua mwenyewe. Watu wengine 27 walijeruhiwa katika hujuma hiyo.

Kansela Merkel alikuwa akizungumza baada ya kikao maalumu cha dharura cha baraza la usalama la mawaziri kilichoitishwa kujadili mashambulizi ya kiholela ya risasi katika jengo la maduka la Olympia mjini Munich na karibu na mgahawa wa vyakula la McDonald.

Merkel amesema mji wa Munich ulikabiliwa na usiku wa hofu na ukatili. "Wakaazi wa Munich wamepitia usiku wa ukatili. Usiku kama huu ni mgumu kwa sisi sote kuuhimili."

"Sote tunaomboleza na mioyo iliyojaa majonzi makubwa, wale wote ambao hawatarejea kwa familia zao. Kwa familia, wazazi na watoto ambao kwao kila kitu leo kinaonekana hakina maana tena, nasema binafsi na kwa niaba ya watu wengi Ujerumani: tunawaunga mkono na tunahisi uchungu pamoja nanyi. Tunawakumbuka, tunawaombea na tunateseka pamoja nanyi."

Aliwapongeza wakazi wa Munich waliowapa hifadhi watu waliokuwa wakimkimbia mshambuliaji, wengi wao wakitumia mitandao ya kijamii kueneza taarifa. Vitendo vyao vilidhihirisha kwamba tunaishi katika jamii huru na vilionyesha ubinadamu, akasema Merkel akiongeza kuwa nguvu zetu kubwa ziko katika maadili haya.

Nach Schießerei in München Bundesinnenminister Thomas de Maiziere
Waziri wa mambo ya ndani, Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Kansela Merkel ameapa kwamba vyombo vya usalama vitafanya kila linalowezekana kuhakikisha umma uko salama na kuulinda uhuru wa kila mtu.

Polisi wamefutilia mbali kuwepo mafungamano kati ya mashambulizi ya Munich na makundi ya itikadi kali za kiislamu na badala yake wanaamini mshambuliaji alikuwa amevutiwa na mauaji ya halaiki na alihamasishwa na mauaji ya kiholela ya nchini Norway miaka mitano iliyopita, ambapo watu 77 waliuliwa na Anders Behring Breivik.

Akizungumzia shambulizi la mjini Munich, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema hakuna ishara yoyote ya mafungamano na ugaidi wa kimataifa.

Viongozi walaani mashambulizi ya Munich

Wakati haya yakiarifiwa viongozi ulimwenguni wametoa rambirambi zao kufuatia mashambulizi ya Munich. Rais wa Marekani Barack Obama amesema Ujerumani mojawapo ya nchi washirika wa karibu na ameahidi kutoa msaada ambao huenda ukahitajika kukabili na kushughulikia halii hii.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault, ameandika katika akaunti yake ya Twitter: "Mshikamano na Ujerumani katika changamoto inayoikabili wakati huu."

"Shambulizi la kigaidi lililowaua watu wengi Munich ni kitendo cha kuudhi kinacholenga kuchochea hofu nchini Ujerumani baada ya mashambulizi katika mataifa mengine ya Ulaya," amesema rais wa Ufaransa, Francois Hollande.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, pia wameungana na Hollande kuelezea wasiwasi wao.

Nach Schießerei in München
Polisi wakipiga doria mjini MunichPicha: picture-alliance/dpa/K.-J. Hildenbrand

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker amesema fikra zao ziko pamoja na wahanga wa mashambulizi ya Munich, familia zao na polisi walioyahatarisha maisha yao kulinda jamii yenye amani. Ulaya nzima sasa iko pamoja na Munich, aliandika Juncker katika akaunti yake ya Twitter. Bendera nje ya majengo ya makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels zimepeperushwa nusu mlingoti.

Iran nayo pia imeyalaani vikali mashambulizi ya Munich ikiahidi msaada katika kuangamiza misimamo mikali inayosababisha machafuko.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier amewashukuru washirika wa kimataifa kwa kauli zao, akisema "ni vyema kufahamu kwamba marafiki zetu Ulaya na ulimwenguni wanatuunga mkono."

Mwandishi:Josephat Charo/rtre,afpe,ap,dpa

Mhariri:Isaac Gamba