1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel and Rutte kuzungumzia ufufuzi wa uchumi wa EU

Tatu Karema
9 Julai 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo anatarajiwa kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte kuzungumzia mchakato wa ufufuaji uchumi wa Umoja wa Ulaya ulioathirika kutokana na janga la Covid-19.

https://p.dw.com/p/3f13Q
Belgien EU-Parlament Angela Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Msemaji wa kansela wa Ujerumani Steffen Seibert, amesema kuwa mazungumzo hayo yatazingatia masuala yatakayopewa kipaumbele na Ujerumani wakati wa muhula wake wa urais wa baraza la Umoja wa Ulaya, wadhifa ambao ni wa kupokezana kati ya mataifa ya Umoja huo.

Macho yote yataelekezwa katika maandalizi ya mkutano maalumu wa kilele wa Umoja wa Ulaya mnamo Julai 17 na 18 ambapo wengi wanatumai kuwepo kwa dalili za makubaliano kuhusu pendekezo la ufufuzi wa uchumi wa Umoja huo la thamani ya euro bilioni 750.Hii inajumuisha msaada wa euro bilioni 500 na mkopo wa euro bilioni 250 kusaidia katika mchakato huo wa ufufuzi wa uchumi.

Mataifa ya Uholanzi, Denmark, sweden na Austria, yanapendelea mikopo badala ya msaada na pesa hizo kutumika katika marekebisho ya kudumu ya kiuchumi. Katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona, Merkel alitoa wito kwa bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels kutafuta mwafaka.

Belgien Brüssel | EU-Ratspräsidenten | Charles Michel
Rais wa baraza la Ulaya - Charles MichelPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Merkel ameongeza kwamba katika muda wa miezi michache ijayo, kutakuwa na changamoto kubwa kujaribu kudhibiti janga hilo na kukabiliana na athari zake za kiafya, kijamii na kiuchumi.  Na kutokana na hali hiyo, Umoja huo unahitaji makubaliano kuhusu mikakati itakayouwezesha kuwa na uhakika kuhusu mfumo wa kifedha na pia hazina ya ufufuzi wa uchumi.

Lakini hali inatarajiwa kusalia kuwa ngumu huku mataifa makuu yanayopinga mikakati ya ufufuzi wa uchumi wa Umoja huo yakikosa kuhudhuria mkutano huo wa jana. Viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya, watakutana tena katika mkutano huo wa Julai 17 na 18 kujaribu kuafikia mwafaka. Mkutano kama huo ulioandaliwa mwishoni mwa mwezi Juni haukupata makubaliano thabiti.

Kuongeza shinikizo  ya makubaliano kabla ya mkutano huo wa wiki ijayo, Merkel pia alikutana na rais wa bunge la Ulaya David Sassoli, rais wa baraza la Ulaya Charles Michel na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo wa faragha, ilisema kuwa washirika wake walikubaliana kuwa kuafikia makubaliano kuhusu mchakato huo wa ufufuzi wa uchumi wa Umoja wa Ulaya  ni suala kuu la kipaombele la Umoja wa Ulaya katika wiki zijazo.