1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya dhidi ya kumomonyoka demokrasia Ujerumani

Iddi Ssessanga
27 Agosti 2018

Merkel ametetea maadili ya kidemokrasia katika mahojiano kufuatia mkwamo wa msimu wa kiangazi ndani ya serikali yake. Waziri wa ndani Horst seehofer amesema hatarajii mkwano mwingine.

https://p.dw.com/p/33qYt
Angela Merkel im ARD-Sommer-Interview
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari, ulinzi wa jamii za wachache na uhuru wa mahakama, na kulaani miito ya wafuasi wa vuguvugu la mrengo mkali wa kulia la PEGIDA kwa kuitisha maandamano ambamo washiriki wamesikika wakitoa miito ya kuwashambulia wageni, baada ya raia wa kigeni kudaiwa kumuuwa mwanaume wa Kijerumani.

Merkel amesema demokrasia ni zaidi ya kupata wingi wa uwakilishi bungeni, na kwamba inajumlisha ulinzi wa wachache, uhuru wa habari na haki ya kuandamana. "Demokrasia ni mahakama huru", alisema kansela Merkel katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ARD siku ya Jumapili. Alisema ikiwa uhuru wa taasisi hizo haulindwi tena, basi demokrasia itakuwa haijakamilika.

Katika siku za karibuni, majaji nchini Ujerumani wamekosolewa na wanasiasa, hasa kuhusiana na hukumu ilioyotolewa na mahakama ya jimbo la North Rhein Westphalia kuhusiana na kuondolewa nchini kinyume na sheria, kwa Sami A. anaedaiwa kuwa mlinzi wa zamani wa kiongozi wa kundi la Al-Qaeda Osama bin Laden.

Chemnitz Abbruch von Stadtfest
Waandamanaji wa vuguvugu la PEGIDA katika mji wa Chemnitz. Agosti 26, 2018.Picha: picture-alliance/dpa/A. Seidel

Suala la uhuru wa habari pia limemulikwa katika wiki za karibuni baada ya maafisa wa polisi kuwashikilia maripota wa Televisheni wakati wa mkutano wa vuguvugu la PEGIDA katika mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Dresden.

Vuguvugu hilo limeitisha maandamano kwa siku ya pili mfululizo hii leo, baada ya kukusanya watu karibu 800 katika mji wa Chemnitz, ulioko katika jimbo la Saxony. Polisi ililaazimika kuomba msaada kuweka kukabiliana na waandamanaji waliotolea maneno ya kibaguzi wageni na kuanza kuwashambulia kwa chupa watu waliokuwa na muonekano wa kigeni.

Achukuwa msimamo mkali kuhusu pensheni, uhamiaji

Merkel pia alizungumzia suala lililozusha mjdala nchini Ujerumani kuhusu suala la pensheni, ambapo aliiambia televisheni hiyo ya ARD kuwa uamuzi kuhusu pensheni utatolewa hivi karibuni. Hata hivyo kansela huyo alikataa pendekezo kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD, ambacho kinashinikiza kuwepo na uhakika kwamba pensheni zitaendelea kuwa imara hadi mwaka 2040.

"Watu wanatakiwa kufahamu kuwa wanapokuwa wamefanya kazi kwa miaka mingi, kwamba wana pensheni juu ya pato la msingi. Niko katika mchalato wa kuhakikisha kwamba wastafu wote wanagawana katika mafanikio haya."

Alisema haiwezekani kuwatwika mzigo vijana na ndiyo maana kuna haja ya kutafuta urari sahihi na "nitatoa tamko langu pale tutakapokuwa na taarifa na takwimu sahihi," alisema kansela na kukitolea wito chama cha SPD kujiepusha na kusababisha mashaka hadi pale tume ya pensheni itakapotoa mapendekezo yake kwa serikali.

ZDF-Sommerinterview 2018 mit Horst Seehofer
Waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer amesema hatarajii kujirudia kwa mkwamo kuhusu uhamiaji.Picha: picture-alliance/dpa/ZDF/J. Hartmann

Pia alikataa pendekezo jengine la SPD ambalo lingewapa waomba hifadhi waliokataliwa, nafasi ya kutafuta kibali cha kuishi kwa muda mrefu ikwia watapata ajira na wanajumuika vizuri katika jamii ya Ujerumani. Merkel alisema mfumo huo utatuma ujumbe usiyo sahihi, kwamba watu wanaoomba hifadhi wanaweza kubadili njia baada ya kuwasili Ujerumani.

Seehorfer amuunga mkono Merkel

Kansela alipata uungwaji mkono kutoka kwa waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer, ambaye alisema katika mahojiano na televisheni nyingine ya umma ZDF jana, kuwa hatarajii kutakuwa na marudio ya mkwamo serikalini kuhusu sera ya uahmiaji. Alisema serikali sasa itakuwa inafanya maamuzi wiki kwa wiki kuhusu pensheni, bima ya wasio na ajira, kupandisha kodi za pango na sera ya uhamiaji kwa wafanyakazi wenye ujuzi maalumu.

Msimamo mkali wa Seehorfer kuhusu uhamiaji na mapambano ya madaraka na Merkel vilisababisha mgogoro wa kiserikali mwezi Juni na mwanzoni mwa Julai, hadi pale muafaka ulipofikiwa kati ya chama cha Merkel cha CDU, chama cha Seehorfer cha CSU pamoja na SPD.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW/EBU/DPAE - https://bit.ly/2LvUYqK

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman