1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asema muungano wa pande tatu unaweza kufanikiwa

Iddi Ssessanga
3 Novemba 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anaamini vyama vya siasa vinavyojaribu kuunda serikali mpya vinakabiliwa na mazungumzo magumu, lakini vinaweza kupunguza tofauti zao.

https://p.dw.com/p/2mzFo
Fortsetzung der Sondierungsverhandlungen
Picha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

Wakati ambapo washirika wake katika muungano uliopita, chama cha Social Democratic SPD, kimeazimia kwenda katika kambi ya upinzani, Merkel anashinikiza kuunda muungano na watetezi wa mazingira - chama cha Kijani pamoja na kile kinachoelemea upande wa biashara cha Free Democrats FDP, baada a muungano wake wa vyama vya kihafidhina kupoteza kura nyingi kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative für Deutschland AfD katika uchaguzi wa mwezi Septemba.

 

"Nadhani kwamba tunakabiliwa na mazungumzo magumu katika siku zijazo lakini pia nadhani bado tunaweza kufikia muafaka ikiwa tutafanya juhudi katika namna ambayo kila mshirika anaweza kuleta utambulisho wake ili kuunda kitu kizuri kwaajili ya taifa zima," alisema Merkel katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin.

Alisema chama cheka cha CDU kwa namna yoyote iko tayari kufanya hilo katika moyo huu," kabla ya kuingia katika awamu nyingine ya mazugumzo.

Balkon-Galerie Jamaika-Sondierungsgepräche
Merkel na wenzake wakiwa katika picha ya pamoja na viogozi wa chama cha Kijani - Die Grüne mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Hatari ya uchaguzi mpya

Merkel anahitaji kuunda muungano ambao haujawahi kujaribiwa kwa ngazi ya taifa, ili aweze kuanza tena kazi, vinginevyo anaweza kushuhudia uongozi wake ukifikia tamati baada ya miaka 12. Kushindwa kwa mazungumzo hayo kunaweza kupelekea kuitishwa uchaguzi mpya, ambao yumkini ukakipa mafanikio zaidi chama cha AfD, kilichoingia bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Septemba.

Lakini baada ya wiki mbili za mazungumzo, washirika wenye mitazamo tofauti wanaedelea kusigana, hususani kuhusu masuala ya uhamiaji, mazingira, usafiri na sera ya kigeni. "Tumekaa pamoja kwa siku 10, mada 12. Matokeo ni nyaraka nane zenye orodha ndefu ya upinzani," alisema Juergen Trittin, mwakilishi wa chama cha Kijani katika mazungumzo na shirika la utangazaji la umma ARD, na kuongeza kuwa katika maeneo manne, hawajaweza kukubaliana hata juu ya nini wanachotofautiana.

Merkel alisema usiku wa siku ya uchaguzi wa Spetemba 24, kwamba ana imani kutakuwa na serikali imara kabla ya siku ya X-mas. Maafisa wa juu katika muungano wake wa kihafidhina, sasa wanasema huenda ikachukuwa hadi mwakani kwa serikali mpya kuweza kuundwa.

Uwezekano wa mazungumzo kufanikiwa

Fortsetzung der Sondierungsgespräche
Mwenyekiti wa FDP Christina Lindner.Picha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

Kiongozi wa chama cha FDP Christian Lindner, anaweka uwezekano wa kufanikiwa kwa mazugumzo hayo kwa asilimia 50-50. Baada ya chama chake kushindwa kupata kiti chochote katika bunge lililopita, ana wasiwasi kuhusu kuridhia mambo ambayo yanaweza kukirejesha tena chama chake katika mashaka kisiasa.

Mtaalamu wa sera ya kigeni wa chama cha Kijani Omid Nouripour, alisema mazugumzo ya kuunda serikali yanaweza kushindwa kiujumla. Chama cha Kijani kipanga kuwasilisha matokeo ya mazungumzo ya awali kwa wanachama wake Novemba 25, ambapo baada ya hapo makundi hayo matatu yanalenga kuhamia kwenye mazungumzo ya kina zaidi.

Merkel amesema wiki mbili za mazungumzo ya kutafuta muafaka zimewaruhusu kujenga misimamo na kuanza kufanyakazi kuelekea makubaliano ya mwisho.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman