1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ataka operesheni ya kuokoa wahamiaji ianze tena

Bruce Amani
16 Agosti 2019

Miezi kadhaa baada ya operesheni ya Umoja wa Ulaya ya uokozi wa wahamiaji katika Bahari ya Mediterania kusitishwa, Kansela Angela Merkel ametoa wito wa operesheni hiyo kuanzishwa tena.

https://p.dw.com/p/3O1xy
Europa Symbolbild Grenzschutzmission "Sophia" rettet weniger Menschen
Picha: picture-alliance/dpa/G. Lami

Tangu mwaka wa 2015, maelefu ya wahamiaji waliokolewa na meli za wanamaji za Umoja wa Ulaya kama sehemu ya mpango wa umoja huo kupambana na usafirishaji wa binaadamu maarufu kama "Operation Sophia,” ambayo ilisitisha shughuli zake mapema mwaka huu.

Akizungumza mjini Berlin, Kansela Merkel amesema ingekuwa vizuri kama hii leo Operation Sophia na wanamaji wa mataifa wanachama wangeendelea na shughuli za uokozi. Aliongeza kuwa operesheni hiyo itasaidia kupunguza wahamiaji pamoja na kupambana na biashara haramu ya kusafirisha watu.

Kansela huyo wa Ujerumani pia alizungumzia uungwaji mkono wake kwa operesheni hizo za uokozi wa majini katika kikao kimoja cha cha mjadala Jumanne iliyopita kaskazini mwa Ujerumani, akizitaja kuwa shughuli za lazima za kiutu. Hayo ni kwa mujibu wa magazeti ya Redaktionsnetzwerk Deutschland.

Merkel hata hivyo amesisitiza kuwa kushughulikia sababu kuu za uhamiaji ni suala la kipaumbele kwa sababu suala la kuwaokoa wahamiji litaendelea kuwepo kama mazingira barani Afrika hayataimarika.

Italien Regierungskrise | Innenminister Matteo Salvini in Rom
Matteo Salvini anakosoa sera za uhamiajiPicha: picture-alliance/Zuma Press/LaPresse/R. Monaldo

"Sio kila wakati ni masikini tu na wanyonge ndio wanaokuja. Tunazungumza na nchi za Kiafrika kuhusu tunachoweza kufanya ili kusaidia. Hatutaki kuwasaidia wasafirishaji watu na wafanabiashara haramu.

Kuna uungwaji mkono imara nchini Ujerumani wa operesheni za wahamiaji na wakimbizi. Uchunguzi wa maoni mwezi uliopita ulionyesha kuwa asilimia 64 ya watu waliohojiwa wanaamini kuwa haikuwa sahihi kwa Umoja wa Ulaya kusitisha operesheni ya uokozi baharini, wakati asilimia 72 wakisema wanaunga mkono meli za uokozi za mashirika yasiyo ya kiserikali.

Italia ilipinga Operesheni Sophia kwa misingi kuwa wahamiaji waliookolewa waliletwa mahususi katika bandari za Italia na kutishia kuzuia operesheni hiyo kama kanuni hazingebadilishwa. Pia iliyataka mataifa mengine  kuwachukua wahamiaji zaidi wanaowasili katika fuo zake. Ujerumani iliunga mkono kwa dhati kuendelea kwa operesheni hiyo ya jeshi la majini.

Wakati huo huo, Italia imewachukua wahamiaji watatu wagonjwa waliokuwa kwenye meli ya uokozi iliyotia nanga kwenye pwani ya Lampedusa, wakati hali ya sintofahamu ikiendelea kutawala juu ya boti hiyo iliyokaa majini kwa wiki mbili sasa licha ya makubaliano ya Umoja wa Ulaya ya kuwachukua watu 134 waliosalia.

Shirika la misaada ya Uhispania la Proactiva Opens Arms, lilisema kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba wahamiaji hao waliokuwa na maradhi yaliyohitaji uangalizi wa kitaalamu pamoja na watu wa kuwasindikiza walipelekwa hadi kwenye kisiwa cha kusini mwa Itali cha Lampedusa jioni ya jana.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Zainab Aziz