1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ataka usitishaji mapigano Ukraine

23 Agosti 2014

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema Jumamosi (23.08.2014) mzozo wa Ukraine unaweza kutatuliwa lakini iwapo tu udhibiti utaimarishwa kwenye mipaka ya Ukraine na Urusi.

https://p.dw.com/p/1CzmR
Kansela Angela Merkel na Rais Petro Poroschenko mjini Kiev. ( 23.08.2014)
Kansela Angela Merkel na Rais Petro Poroschenko mjini Kiev. ( 23.08.2014)Picha: Reuters

Merkel ambaye ametaka pande zote mbili kusitisha mapigano mashariki kwa Ukraine ambapo waasi wamekuwa wakipambana na vikosi vya serikali amesema kufuatia mazungumzo yake na Rais Petro Poreshenko wa Ukraine kwamba kuheshimiwa kwa mipaka ya Ukraine ni lengo la sera ya kigeni ya Ujerumani.

Pia ametangaza hatua za kifedha zenye lengo la kusaidia sekta za nishati na maji za nchi hiyo na kupunguza masahibu ya wakimbizi.

Merkel anaitembelea Kiev ikiwa ni siku tatu kabla ya mkutano wa wiki ijayo kati ya Rais Poreshenko wa Ukraine na Rais Vladimir Putin wa Urusi uliopangwa kufanyika nchini Belarus ambao wanadiplomasia wanasema ni fursa nzuri kuwahi kujitokeza kwa miezi kadhaa ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani mashariki mwa Ukraine ambako vikosi vya serikali vinapambana na waasi wanoegemea upande wa Urusi.

Wakati Merkel akiwasili nchini humo Jumuiya ya Kujihami ya NATO imedai kwamba jeshi la Urusi liko nchini Ukraine likiwasaidia waasi na serikali ya Urusi ikiighadhibisha serikali ya Ukraine na washirika wake wa mataifa ya magharibi kwa kutuma msafara wa malori yenye kubeba misaada nchini Ukraine dhidi ya matakwa ya serikali ya nchi hiyo.

Matumaini ya amani

Merkel akiuwekea matumaini mkutano wa Jumanne kati ya Putin na Poroshenko amekaririwa akisema " Lazima kuwepo na pande mbili ili kuweza kufanikiwa.Huwezi kufikia amani wewe mwenyewe tu.Natumai mazungumzo na Urusi yatazaa mafanikio."

Kansela Angela Merkel na Rais Petro Poroschenko mjini Kiev. ( 23.08.2014)
Kansela Angela Merkel na Rais Petro Poroschenko mjini Kiev. ( 23.08.2014)Picha: Reuters

Kiongozi huyo wa Ujerumani amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Poroshenko katika mji mkuu wa Ukraine,Kiev kwamba mipango iko mezani na sasa vitendo lazima vifuatie.

Amesema usitishaji wa mapigano unahitajika lakini kikwazo kikuu ni ukosefu wa udhibiti kwenye mpaka wa kilomita 2,000 kati ya Ukraine na Urusi.Amependekeza serikali za nchi hizo mbili zikubali kufikia makubaliano kwa mpaka huo kusimamiwa na waangalizi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE).

Vita sio chaguo lao

Kwa upande wake Poroshenko amesema "Vita sio chaguo lao bali vimelazimishwa kwao kutoka nje."

Mizinga ya vikosi vya serikali nje ya mji wa Donetsk.
Mizinga ya vikosi vya serikali nje ya mji wa Donetsk.Picha: picture-alliance/AP Photo

Amesema upande wa Ukraine na washirika wao wa mataifa ya magharibi watafanya kila wawezalo kuleta amani lakini sio kwa gharama ya haki ya kujitawala kwa dola, kuheshimiwa kwa mipaka yake na uhuru wa Ukraine.

Masaa machache kabla ya ndege ya Merkel kutua mjini Kiev, kulikuwa na mashambulio mazito ya mizinga mjini Donetsk ngome kuu ya waasi mashariki mwa Ukraine karibu na mpaka na Urusi.Waandishi wa shirika la habari la Uingereza Reuters wameshuhudia majengo yakiharibiwa na madimbwi ya damu ambapo kwa mujibu wa wakaazi wa mji huo raia wawili wameuwawa.

Mashambulizi hayo mazito ya mizinga ambayo sio ya kawaida yumkini ikawa ni shinikizo la vikosi vya serikali kupata ushindi dhidi ya waasi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Ukraine ambayo inaangukia Jumapili.

Dhamira ya ziara ya Merkel

Wanadiplomasia wanasema Merkel ana dhamira mbili katika ziara yake hiyo fupi huko Kiev ambapo kimsingi ni kuonyesha kuiunga mkono serikali ya Ukraine katika mzozo wake na Urusi lakini pia kumhimiza Poroshenko kuwa tayari kuzingatia mapendekezo ya amani wakati atakapokutana na Putin wiki ijayo.

Msafara wa malori ya Urusi yenye kubeba msaada yakielekea Donetsk,Ukraine. (21.08.2014)
Msafara wa malori ya Urusi yenye kubeba msaada yakielekea Donetsk,Ukraine. (21.08.2014)Picha: Reuters

Ziara ya Merkel inakuja siku moja baada ya Urusi kupeleka msafara wa malori yenye kubeba msaada mashariki mwa Ukraine na kuzusha shutuma kutoka serikali ya Ukraine kwamba ni uvamizi wa moja kwa moja wa ardhi yake shutuma ambazo zimeungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya NATO,Marekani na Umoja wa Ulaya.

Serikali ya Urusi imesema msafara huo umeingia Ukraine bila ya kibali cha serikali ya nchi hiyo kutokana na kwamba raia walioko kwenye maeneo hayo yaliozingirwa na vikosi vya serikali wako katika hali mbaya ya kuhitaji msaada wa dharura wa chakula,maji na mahitaji mengine.

Mzozo huo wa Ukraine umeuweka uhusiano kati ya Urusi na mataifa ya magharibi katika hali mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea kumalizika kwa Vita Baridi na kuzusha mlolongo wa vikwazo vya kibiashara ambavyo vinaathiri uchumi ulio tayari dhaifu barani Ulaya na nchini Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa/AFP

Mhariri : Iddi Ssessanga