1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atetea kauli yake kuhusu Marekani, Uingereza

Iddi Ssessanga
29 Mei 2017

Matamshi ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwamba Ulaya haiwezi tena kuzitegemea Marekani na Uingereza kama washirika wa kutumainiwa yamepokelewa kwa hisia ndani ya Ulaya na kanda ya Shirika la kujihami la NATO.

https://p.dw.com/p/2dme5
Belgien Nato-Gipfel | Trump und Merkel
Picha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Merkel amezikasirisha Washinton na London kwa kusema Jumapili kwamba Ulaya inapaswa kubeba hatma yake mikononi mwake, akimaanisha kuwa Marekani chini ya Rais Donald Trump na Uingereza baada ya kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya hazikuwa tena washirika wa kutegemewa.

Aliyatoa matamshi hayo baada ya Trump kuwakosoa washirika muhimu wa jumuiya ya kujihami NATO kuhusiana na matumizi yao ya kijeshi, na kukaataa kuidhinisha makubaliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika mikutano ya kilele iliofuatana juma lililopita.

Bado ni mkereketwa wa kanda ya Atlantiki

Akizungumza katika mkutano wa kawaida na serikali na waandishi habari mjini Berlin, msemaji wa serikali Steffen Seibert amesema matamshi ya kansela yanansimama kivyake, yalikuwa dhahiri na yanaeleweka, na kuongeza kuwa alikuwa muumini mkubwa wa kanda ya atlantiki aliezungumza.

NATO Donald Trump Belgien Mimik
Rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May wakati wa mkutano wa kilele wa NATO mjini Brussels.Picha: Getty Images/J.Tallis

Baada ya mikutano ya kilele ya jumuiya ya NATO na G7, Merkel aliuambia mkutano mjini Munich kwamba enzi ambapo Ulaya ingewategemea kikamilifu wengine zimepita kwa kiasi fulani. "Sisi watu wa Ulaya tunapaswa kuweka mustabali wetu mikononi mwetu - bila shaka tukiwa na urafiki na Marekani, Uingereza, na inapowezekana, pia urafiki na Urusi na nchi nyingine," alisema Merkel.

Akizungumza Jumatatu katika mkutano kuhusu maenedeleo endelevu mjini Berlin, Merkel alirejea kauli yake na kusema ilikuwa sahihi kutomumunya maneno kuhusu tofauti na Marekani, na kuongeza kuwa mjadala wakati wa mkutano ya G7 ulionyesha kuwa itakuwa vigumu kuyatekeleza makubaliano yaliofikiwa mjini Paris.

Mapokezi mchanganyiko Marekani

Nchini Marekani, kulikuwa na hisia mchanganyiko kuhusu matamshi ya Merkel, ambapo wafuasi wa Trump waliyapuuza matamshi hayo wakati wapinzani wake walionekana kuomboleza kupotea kwa uhusiano maalumu kati ya Marekani na Ujerumani.

Mbunge wa chama cha Democratic Adam Schiff ambaye pia ni mjumbe wa juu wa kamati ya upelelezi ya bunge, alisema "ikiwa rais wa Marekani anaitaja ziara yake kuwa yenye ufanisi mkubwa, anahofia kuona kushindwa.

G7 Gipfeltreffen Donald Trump spricht mit Angela Merkel und Beji Caid Essebsi
Merkel akiteta jambo na Trump wakati wa mkutano wa kilele wa G7 mjini Taormina, Sicily, ItaliaPicha: Reuters/J. Ernst

Lakini wafuasi wa Trump wameyachukulia matamshi ya Merkel kama ishara ya mafanikio ya rais wao. Bill Mitchel, mtangazaji wa kihafidhina aliepewa jina na naibu wa Trump wa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya Marekani, alitumia fursa hiyo kumkashifu Merkel, akisema katika ukurasa wake wa twita kuwa: Merkel, shujaa wa mrengo wa kushoto aliekumbwa na majanga barani Ulaya, anasema hawezi kumtegemea Trump. Inachekesha. Anapinga upumbavu wako!

London bado ni mshirika wa kutegemewa

Nchini Uingereza waziri wa mambo ya ndani Amber Rudd aliiambia redio ya BBC kuwa licha ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, kanda hiyo inaweza kuendelea kuitegemea London kama mshirika.

Lakini Guy Verhofstadt, mbunge wa bunge la Ulaya na kiongozi wa majadiliano ya Brexit kwa upande wa bunge la Ulaya, alismea mabadiliko katika uhusiano wa miongo kadhaa hayahitaji kuharibu mustakabali wa kanda hiyo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtrr,dpae,afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman