1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel azuru Afrika Kusini na Angola

Amina Mjahid
6 Februari 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel yupo katika ziara ya siku mbili nchini Afrika Kusini na Angola inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/3XMhT
Südafrika Angela Merkel und Cyril Ramaphosa
Picha: Reuters/S. Sibeko

Ziara hiyo ya kansela Merkel barani Afrika imeanzia Afrika Kusini kwa mazungumzo ya biashara, uwekezaji na ushirikiano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo mataifa yote mawili yanahudumu kwa mihula ya miaka miwili. Afrika Kusini ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Ujerumani barani Afrika huku Ujerumani ikiwa mshirika wa pili mkubwa wa kibiashara Afrika Kusini baada ya China.

Rais Ramaphosa, amesema taifa lake linatarajia kujifunza  kwa Ujerumani kutoka katika matumizi ya makaa ya mawe hadi katika matumizi ya nishati mbadala ili kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na tatizo la umeme nchini humo. 

Rais huyo wa Afrika Kusini ametoa wito pia wa biashara  zaidi za ujerumani kuwekeza nchini Afrika Kusini, kuongezea kwenye biashara nyingine 600 za ujerumani zilizopo nchini humo, ambapo asilimia 30 ya watu wake hawana ajira.  Kansela Merkel amesema kuna masuala kadhaa yanayohitaji kushughulikiwa ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji

Besuch von Bundeskanzlerin Merkel in Südafrika
Kansela Merkel ameongozana na ujumbe wa wafanyabiashara kwenye ziara hiyoPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

"Merkel ((Najua kwa upande wenu kwamba kila kitu kinatekelezwa ili kukaribisha wawekezaji. Wajumbe wa bishara niliokuja nao wanataka kuwekeza. Na wakati mwingine yanakuja mabo ambayo tunahitaji kuzungumzia ili kuondoa vikwazo, na nia njema ya pande zote inapelekea matokeo. Ndiyo nafurahi kwamba wafanyabiashara wetu na Afrika Kusini wana fursa ya kutueleza yale yanayowapa tabu, malalamiko yao na tutarudi tukijua zaidi ya tulivyokuja" alisema Merkel.

Viongozi hao wawili pia wamezungumzia  mapigano nchini Libya huku kansela Merkel akisema kuna umuhimu wa kushirikiana katika kutafuta suluhu la kisiasa la taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika bila ya kulazimisha muafaka kwa watu wa Libya.

Afrika kusini hivi karibuni itachukua uwanachama wa kupokezana wa Umoja wa Afrika huku Libya ikiwa ni suala tete la kujadiliwa katika muungano huo. Hata hivyo Angela Merkel amesema masuala mengine yatajadiliwa katika mkutano wa kilele unaokuja wa Umoja wa Ulaya  na Mataifa ya Afrika.

Ziara ya Merkel Afrika Kusini imekuja baada ya mkutano wa kilele wa Afrika unaojulikana kama "Compact for Africa" uliofanyika mjini Berlin. Katika ziara hii Merkel ameandamana na ujumbe wa wafanya biashara wa Ujerumani.