1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Haki na uhuru Hong Kong vilindwe

6 Septemba 2019

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema Ijumaa kuwa haki na uhuru wa raia wa Hong Kong ni sharti vilindwe na suluhisho la mzozo wa kisiasa katika mji huo wa China linaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo.

https://p.dw.com/p/3PAGF
China: Bundeskanzlerin Merkel in Peking
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Akiwa kwenye siku ya pili ya ziara yake nchini China, Kansela huyo wa Ujerumani amesema machafuko yanastahili kuepukwa kwa njia yoyote ile.

Merkel amekutana na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang baada ya kuwasili Beijing Ijumaa asubuhi. Anatarajiwa kukutana na Rais Xi Jinping baadae Ijumaa kwa chakula cha jioni.

Machafuko yanastahili kuepukwa kwa njia yoyote ile

Kiongozi huyo wa Ujerumani anakabiliwa na changamoto ya kuzungumzia wasiwasi wa ukiukaji wa haki za binadamu na mazungumzo ya kiuchumi na mojawapo ya washirika wakubwa wa kibiashara wa Ujerumani.

China: Bundeskanzlerin Merkel in Peking
Kansela Angela Merkel (aliyeketi) na Waziri Mkuu Li Keqiang wa ChinaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

"Katika hali iliyoko sasa, machafuko yanastahili kuepukwa kwa njia yoyote ile na suluhisho linaweza kupatikana tu kwa njia ya kisiasa - hivyo ni kusema kupitia mazungumzo. Kuna ishara pia kwamba mkuu wa Hong Kong anataka kuwaalika watu kwenye majadiliano na natumai kutakuwa na majadiliano kwa kuwa naichukulia hiyo kama hatua muhimu sana. Natumai kwa msingi huu wale ambao wamekuwa wakiandamana watashiriki mazungumzo hayo," alisema Angela Merkel.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Li Keqiang amesema China itausitisha mzozo wa Hong Kong kupitia sheria tu. Li ambaye amezungumzia kwa mara ya kwanza suala la mzozo huo wa Hong Kong ambao unagonga vichwa vya habari vya kimataifa na kuiwekea shinikizo China, amesema nchi hiyo ina hekima ya kuudhibiti mzozo huo kwa misingi ya sheria.

Kuna wasiwasi wa China kutuma majeshi Hong Kong

"Tunaunga mkono serikali ya eneo hilo maalum lenye utawala wake wa ndani kusitisha machafuko, kudhibiti maandamano na kurudisha amani kulingana na sheria. Haya ni kwa ajili ya ustawi na amani ya siku zijazo ya Hong Kong. Tunastahili kuwa na imani kwamba China inaweza kuyasuluhisha mambo yake," alisema Li Keqiang.

Bundeskanzlerin Merkel in China
Kansela Merkel na Li Keqiang wakizungumza na waandishi wa habariPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kumekuwa na wasiwasi katika siku za hivi karibuni kwamba China inaweza kuwatuma wanajeshi iwapo serikali ya Hong Kong itatuma ombi kwa ajili ya kuyasitisha machafuko yanayoendelea katika mji huo ambao kwa kiasi fulani unajitawala wenyewe.

Merkel ambaye yuko kwenye ziara ya siku tatu China ameelezea kuridhishwa kwake na hatua ya Hong Kong kuondoa mswada wa kuhamishwa kwa watuhumiwa kwa ajili ya kuhukumiwa China, jambo mojawapo ambalo limekuwa likipingwa pakubwa na waandamanaji.

Viongozi wa maandamano hayo walikuwa wametoa wito wa kukutana na Merkel ingawa msemaji wa Kansela huyo amesema kiongozi huyo hana mpango wa kukutana nao.