1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel haondowi uwezekano wa kuzuia mradi wa gesi na Urusi

Mohammed Khelef
7 Septemba 2020

Kansela Angela Merkel asema hajaondosha uwezekano wa kuzuwia mradi wa bomba la gesi ambalo litaiwezesha gesi ya Urusi kufika barani Ulaya, Nord Stream 2, kama adhabu kuhusu kisa cha Alexei Navalny.

https://p.dw.com/p/3i7KY
Deutschland Merkel PK Navalny
Picha: Getty Images/AFP/M. Schreiber

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hajaondosha uwezekano wa kuzuwia uendelezaji wa mradi wa bomba la gesi ambalo litaiwezesha gesi ya Urusi kufika barani Ulaya, maarufu kama mradi wa Nord Stream 2, kama hatua ya kuiadhibu Urusi kwa tuhuma za shambulio la sumu dhidi mpinzani mkuu wa Rais Vladimir Putin, Bwana Alexei Navalny, ambaye anaendelea kutibiwa mjini Berlin, huku Moscow ikipuuzilia mbali tuhuma kwamba inahusika na shambulio hilo.

Kansela Merkel anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka ndani ya chama chake cha kihafidhina kuusitisha mradi huo mkubwa kabisa wa bomba la gesi kutoka Urusi ambao kwa sasa umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na unaotazamiwa kuanza kazi mapema mwakani.

Alipoulizwa na waandishi wa habari Jumatatu endapo Merkel anakubaliana na waziri wake wa mambo ya kigeni, Heiko Maas, kutokea chama cha Social Democratic, SPD, juu ya usitishwaji wa bomba hilo, msemaji wa Kansela Merkel, Steffen Seibert, alisema kwamba kansela huyo anakubaliana na mawazo yaliyotolewa na Maas.

Kansela Merkel anakabiliwa na shinikizo kubwa kuusitisha mradi wa Nord Stream 2 kufuatia kisa cha kiongozi wa upinzani wa Urusi kupewa sumu.
Kansela Merkel anakabiliwa na shinikizo kubwa kuusitisha mradi wa Nord Stream 2 kufuatia kisa cha kiongozi wa upinzani wa Urusi kupewa sumu.Picha: picture-alliance/Fotostand/freitag

Kauli hiyo imechukuliwa na wachambuzi wa mambo hapa nchini Ujerumani kwamba ni ishara ya wazi kwamba Kansela Merkel yuko tayari kwenda mbali zaidi katika kuiadhibu Urusi kutokana na kadhiya ya Bwana Navalny. Hata hivyo, Seibert alionya kwamba bado ingali mapema mno kuamuwa endapo vikwazo dhidi ya Urusi kwa tukio la Navanly kulishwa sumu vitekelezwe, hasa kutokana na ukweli kwamba mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2, haihusu Ujerumani pekee:

"Linapohusika gesi itakayopitishwa kwenye bomba la Nord Stream 2, gesi hiyo itaingia kwenye miundombinu ya Ulaya. Huu mradi unaitwa wa Ujerumani kwa kuwa unahusisha kampuni nyingi za Kijerumani, lakini utekelezwaji wake ni wa kimataifa ukizihusu nchi nyengine kadhaa za Ulaya."

Hapo jana akizungumza na kituo cha televisheni cha ARD cha hapa Ujerumani, Waziri wa Mambo ya Kigeni Heiko Maas alisema Urusi inapaswa kuelezea kwa uwazi mazingira ya kulishwa sumu kwa Navalny, ama ikabiliwe na uwezakano wa Ujerumani kujiondowa kwenye mradi wa Nord Stream 2.

Alexei Navalny anaendelea kupata matibabu nchini Ujerumani
Alexei Navalny anaendelea kupata matibabu nchini UjerumaniPicha: Reuters/T. Makeyeva

Lakini kwenye majibu yake msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov, ameyaita madai ya Ujerumani kwamba Navalny alilishwa sumu ni ya kipuuzi na ya maudhi, na badala yake akaitaka Ujerumani kuwasilisha kwake ripoti rasmi ya uchunguzi huo uliofanywa na madaktari wa Hospitali ya Cherite mjini Berlin.

Kwa vyovyote vile, hatua ya kujiondowa kwenye mradi wa Nord Stream 2 huenda likawa jambo gumu kabisa kutekelezeka kwa hali ambayo umeshafikia, ingawa Marekani inayopigania kuuza gesi yake Ulaya, ingelipendelea sana kuona hilo likitokea.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/FP
Mhariri: Josephat Charo