1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Schulz kwa mazungumzo

Josephat Charo
30 Novemba 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atafanya mazungumzo ya kwanza leo (30.11.2017) na mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD, Martin Schulz, kuangalia uwezekano wa kuunda serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/2oXzE
Bundestagswahl | Elefantenrunde Schulz und Merkel
Picha: imago/photothek/T. Imo

Mkutano huo unaofanyika chini ya mualiko wa rais wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, unatarajiwa kuanza saa mbili usiku saa za hapa Ujerumani na unatarajiwa kuangalia ikiwa pande hizo mbili ziko tayari kuanza mazungumzo ya serikali mpya. Baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba kumuacha Merkel bila wingi wa wajumbe bungeni, chama cha SPD kilitangaza kwa ukaidi kwamba hakitaendelea kushirikiana na kansela huyo, baada ya kufanya vibaya sana na kupata matokeo ya kuabisha katika uchaguzi huo.

Lakini baada ya juhudi za Merkel kuunda serikali ya mseto na chama cha walinda mazingira cha Kijani na chama cha kiliberali kinachowapendelea wafanyabishara, FDP, kusambaratika, chama cha SPD kilikabiliwa na shinikizo la kubadili msimamo wake ili kuepusha uchaguzi wa mapema.

Jarida linalochapishwa kila wiki hapa Ujerumani, Der Spiegel, limedokeza kwamba mkutano wa leo utakaohudhuriwa pia na Horst Seehofer, mwenyekiti wa chama cha Bavaria cha Christian Social Union, CSU, ni wa umuhimu mkubwa kwa mwanasiasa siasa huyo mkongwe. Kwa kansela Merkel "ni vita vya kupigania mustakabali wake kisiasa ambavyo vinaanza" limesema jarida la Spiegel na kuongeza kuwa Merkel analazimika kufanya kila kitu kuunda muungano huu, ambao pekee utahakikisha mamlaka thabiti.

Akizungumzia mkutano wa leo Schulz amesema kujenga mustakabali mwema kwa Ujerumani ni jukumu la serikali ijayo. Hiyo haina maana kuongoza nchi bila mpango wa muda mrefu. Ina maana kufanya mageuzi muhimu ambayo itabidi yapiganiwe na kujadiliwa kwa kina.

Frank-Walter Steinmeier ASEM Asien Europa Treffen Luxemburg
Rais wa Ujerumani, Frank Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

"Kwa ari nzuri kabisa duniani, siwezi kuwaambia matokeo ya mkutano huu yatakavyokuwa. Naweza kuwahakikishia jambo moja: kwamba nitapigania suluhisho bora linalowezekana kwa taifa hili, ambalo chama changu kinafahamu jukumu lake. Jambo moja ni bayana: Tunahitaji uthabiti, ushirikiano na mabadiliko."

Schulz amekuwa chini ya shinikizo la rais Steinmeier na amebadili msimamo wake wa kutotaka kushiriki katika serikali ya mseto. Ameashiria yuko tayari kujadili njia itakayoisaidia Ujerumani kuondokana na mkwamo wa kisiasa ambao umekuwa ukiikabili kwa miezi miwili sasa.

Kikao chakabiliwa na kiwingu

Mazungumzo ya leo yanagubikwa na wingu la kisiasa lililosababishwa wiki hii na mwanachama wa chama cha kihafidhina cha CDU, waziri wa kilimo Christian Schmidt, ambaye alivuka mpaka wa serikali yake na kupiga kura kuunga mkono dawa ya kuua magugu, glyphosite, yenye utata wakati wa kutano wa Umoja wa Ulaya. Hatua hiyo ambayo Schmidt anasema aliichukua peke yake, ilikosolewa kama uvunjaji wa uaminifu na chama cha SPD, ambacho kimekuwa mshirika mdogo katika serikali ya kansela Merkel tangu mwaka 2013.

Huku Merkel akijaribu kukishawishi chama cha SPD, hatua ya waziri Schmidt yumkini ikasababisha athari kubwa kwa mahafidhina. Carsten Linnemann anayeliongoza shirika la kampuni ndogo na za wastani la chama cha CDU, amesema suala hili bila shaka litakuwa kikwazo katika mazungumzo ya leo.

Carsten Schneider, kiongozi wa chama cha SPD bungeni amekiambia kituo cha televisheni cha ARD kwamba tukio hilo linaonyesha Merkel hana udhibiti wa jinsi mambo yanavyoendeshwa katika chama chake. Na licha ya kwamba Schulz amekubali kukaa katika meza ya mazungumzo na Merkel, mpaka sasa hajaahidi chochote kuhusu uwezekano wa kuundwa serikali nyingine ya mseto ya mrengo wa kulia na kushoto.

Kansela Merkel amesita kuunda serikali isiyo na wingi bungeni kutokana na kuyumba kwa serikali ya aina hiyo. Lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Ujerumani vikivinukuu vyanzo ambavyo havikutambuliwa vimeripoti kwamba sasa anapendelea chaguo hilo badala ya kufanya uchaguzi wa mapema, iwapo mazungumzo na chama cha SPD yatagonga mwamba.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/retuers/dpae

Mhariri:Yusuf Saumu