1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Cameron wajadili biashara na Umoja wa Ulaya

Admin.WagnerD8 Januari 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kumsaidia waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kulitatua tatizo la watu wanaotumia vibaya mfumo wa nchi hiyo wa malipo ya uzeeni na msaada kwa wasiojiweza.

https://p.dw.com/p/1EGaU
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini London
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini LondonPicha: picture alliance/AP Photo/J. Stillwell

Ahadi ya Kansela Angela Merkel ilifuatia kauli ya mwenyeji wake, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, kuhusu tatizo la wahamiaji kutoka nchi za Umoja wa Ulaya wanaoingia nchini mwake, na kuulemea mfumo wa nchi hiyo wa malipo ya uzeeni na kuwasaidia watu wasiojiweza, hali ambayo alisema imewakasirisha raia wengi wa Uingereza na kuzorotesha uhusiano kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, Cameron alisema anaamini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.

Pamoja na imani hiyo lakini, waziri mkuu huyo wa Uingereza alisema anayo matumaini kuwa Umoja wa Ulaya utafanyiwa mageuzi. David Cameron anakabiliwa na shinikizo la chama cha UKIP ambacho kinaupinga Umoja wa Ulaya, huku uchaguzi mkuu wa mwezi Mei ukikaribia.

Bi Merkel asisitiza uhuru wa kutembea

Akitoa jibu kwa wasiwasi huo wa Uingereza, Bi Merkel amesema tatizo lililopo litashughulikiwa, bila lakini kuukwaza uhuru wa watu kwenda wanakotaka.

Alisema, ''Ama kuhusu uhuru wa watu kwenda watakako, kama tulivyosema mimi na David Cameron hilo siyo suala la mjadala, lakini inatubidi kuwashughulikia wale wanaoutumia vibaya uhuru huo. Tunatafakari hatua za kisheria, na inatubidi kuzieleza mamlaka husika katika kila nchi kwamba matumizui hayo mabaya ya uhuru hayana budi kushughulikiwa ili kuudumisha uhuru huo''.

Kansela Merkel amesisitiza uhuru wa raia wa Umoja wa Ulaya kwenda watakako ndani ya umoja huo
Kansela Merkel amesisitiza uhuru wa raia wa Umoja wa Ulaya kwenda watakako ndani ya umoja huoPicha: Fotolia/chrisdorney

Bi Merkel pia alizungumzia uwezekano wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, akisema hilo likitokea litakuwa pigo kubwa kwa Ulaya, na kuongeza lakini kuwa litakuwa pigo kubwa zaidi kwa Uingereza.

Kero za Uingereza lazima zijibiwe

Ikisalia miezi minne hadi kufanyika uchaguzi mkuu nchini Uingereza, suala la nchi hiyo kuondoa uanachama wake kwa Umoja wa Ulaya linazidi kuzungumziwa. Katika mkutano wa pamoja na kansela Merkel mbele ya waandishi wa habari, Waziri Mkuu Cameron alisema katika kuushughulikia uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, maslahi ya nchi yake yatapewa kipaumbele.

''Ninayo nia ya kuupata ufumbuzi katika uhusiano kati yetu na Ulaya, na kama tulivyosema pamoja na Kansela Merkel, penye nia pana njia, na hayo ndiyo maoni yangu pia. Ni katika kufikia kile ambacho ni maslahi ya muda mrefu kwa Uingereza, na pia, naamini hivyo, kwa Umoja wa Ulaya.'' Alisema Cameron.

Mbali na suala la uhusiano baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya, viongozi hao wawili walilaani vikali mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jarida la kila wiki mjini Paris, Ufaransa jana ambapo watu 12 waliuawa, wakiliita shambulizi hilo kuwa la kinyama, na kuelezea mshikamano wao na watu wa Ufaransa.

Hali kadhalika waligusia masuala mengine yenye umuhimu, kama vile uchaguzi ujao nchini Ugiriki na hatima ya nchi hiyo katika umoja wa sarafu ya Euro, na maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika Magharibi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/ DW Website-English

Mhariri: Iddi Ssessanga