1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Steinmeier ni miongoni mwa walioathirika na udukuzi

Sylvia Mwehozi
4 Januari 2019

Mamlaka za Ujerumani zinachunguza kisa cha kuibiwa kwa mamia ya data za taarifa za wanasiasa akiwemo Kansela Angela Merkel na namna taarifa hizo zilivyoweza kudukuliwa na kuanikwa mtandaoni. 

https://p.dw.com/p/3B2w1
Deutschland Totenmesse für Kohl in Berlin
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Macdougall

Msemaji wa serikali,  Martina Fietz, amesema Kansela Merkel ni miongoni mwa walioathirika na aliarifiwa juu ya shambulio hilo Alhamis jioni. Data hizo zinazojumuisha anuani za nyumbani, namba za simu, barua, na vitambulisho zilichapishwa kwenye mtandao wa Twitter kuanzia mwezi Desemba mwaka uliopita lakini zimekuja kujulikana wiki hii.

Kama mnavyofahamu, sasa inajulikana kwamba data binafsi na nyaraka za mamia ya wanasiasa na watu maarufu zimechapishwa mtandaoni. Katika uwanja wa siasa, uchambuzi wa awali unaonyesha wanasiasa na wawakilishi katika ngazi zote wameathirika, ikiwemo bunge la Ulaya, bunge la Ujerumani Bundestag, mabunge ya majimbo, pamoja na wawakilishi wa mikoa. Mamlaka zinafanya kazi kubaini kiwango na kisa cha tukio hili na kutoa usaidizi kwa walioathirika, alisema Martina.

Taarifa zaidi zinasema manaibu kutoka vyama vyote walio na uwakilishi kwenye bunge la shirikisho wamedukuliwa pamoja na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Hata hivyo msemaji wa serikali amesema uchunguzi wa awali unaashiria kwamba "hakuna taarifa nyeti au data" kutoka ofisi ya kansela kati ya zilizodukuliwa. Ingawa ameonya kwamba baadhi ya nyaraka zilizoibwa na taarifa zinaweza kutumiwa vibaya.

Deutschland Fragestunde im Bundestag
Bunge la Ujerumani ambalo limeathirika na udukuzi wa dataPicha: picture-alliance/AA/A. Hosbas

Kituo cha redio cha umma cha RBB kilikuwa cha kwanza kuripoti juu ya udukuzi huo. Akaunti ya Twitter ambayo imechapisha taarifa hizo ilikuwepo wazi mtandaoni hadi majira ya mchana siku ya Ijumaa kabla haijafungiwa na Twitter na ilikuwa na wafuasi 17,000.

Kiungo kilicho ambatanishwa kiliashiria kwamba taarifa za wanasiasa kutoka vyama vyote bungeni kasoro chama mbadala kwa Ujerumani AfD, zilianza kuchapishwa kabla ya Krismasi. Hata hivyo shirika la usalama wa mtandao la serikali limesema mtandao wa serikali haukuathirika. Mbali na wanasiasa, udukuzi huo pia umewalenga watu maarufu na waandishi wa habari.

Ujerumani imeshuhudia mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya mifumo ya kompyuta ya serikali na bunge katika miaka ya hivi karibuni. Serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito mkubwa. Hadi sasa haijawa wazi ikiwa udukuzi huo ulitekelezwa na wahalifu au ni matokeo ya kuvuja kwa data kutoka ndani. Ofisi ya shirikisho inayohusika na usalama wa taarifa sambamba na taasisi ya ujasusi ya ndani wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef