1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi azomewa na mashabiki wa PSG uwanjani

3 Aprili 2023

Masaibu ya staa wa Argentina na klabu ya Paris St Germain Lionel Messi bado yanaendelea baada ya PSG kupokea kichapo cha 1-0 mbele ya mahasimu wao Olympique Lyon jana Jumapili ugani Parc de Princess.

https://p.dw.com/p/4PePZ
Fußball Champions League | Paris Saint-Germain - FC Bayern München
Picha: Christian Kolbert/kolbert-press/IMAGO

Jina la Lionel Messi lilizomewa na mashabiki wa Paris St Germain uwanjani Parc des Princess kabla ya kuanza kwa mechi kati yao na Lyon kufuatia tetesi kwamba huenda akarudi Barcelona.

Kelele za mashabiki zilizidi kuhanikiza baada ya kichapo cha 1-0, bao lililofungwa na Bradley Barcola kunako dakika ya 56 na kuzima kabisa matumaini ya PSG.

Kipigo hicho kilikuwa chao cha tano msimu huu katika Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1 na kushuhudia uongozi wao ukipungua hadi alama sita kati yao na Lens, inayoshikilia nafasi ya pili. Marseille ni ya tatu ikiwa na alama 60 huku Monaco ikifunga ukurusa wa timu nne bora za Ligue 1.

Paris St Germain tayari imeondolewa kutoka Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na pia Kombe la Ufaransa na kumuacha kocha Christophie Galtier katika hali mbaya ya kuhifadhi kibarua chake.

Nyota huyo mshindi wa Kombe la Dunia, anakaribia mwisho wa mkataba wake wa miaka miwili na klabu hiyo ya mjini Paris.

Licha ya mazungumzo kuanza juu ya kuongeza mkataba huo, kuna tetesi kwamba huenda akarudi tena katika maskani yake ya zamani ya Nou Camp.

Makamu wa rais wa Barcelona Rafael Yuste, amefichua kuwa klabu hiyo imeanzisha mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35.

"Messi anajua jinsi tunavyomthamini. Ningependa arudi Barcelona. Tunawasiliana na wawakilishi wake, hilo halina shaka."