1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi na babake wafika kizimbani

27 Septemba 2013

Nyota wa Barcelona Lionel Messi na babake wamefika katika mahakama moja ya Uhispania kujibu mashitaka yanayohusiana na kesi ya kukwepa kulipa kodi ya mamilioni ya euro

https://p.dw.com/p/19peJ
Lionel Messi na babake Jorge Horacio Messi wakiingia katika mahakama ya Gava, kusini mwa Barcelona
Lionel Messi na babake Jorge Horacio Messi wakiingia katika mahakama ya Gava, kusini mwa BarcelonaPicha: Reuters

Messi alitoa majibu kwa takribani nusu saa baada ya babake Jorge Horacio Messi kuulizwa maswali. Baada ya wote wawili kuondoka mtu na njia yake, wakili wa Messi alizungumza nje ya chumba cha mahakama hiyo ya mjini Gava, kusini mwa Barcelona, karibu na makaazi ya Messi. Wakili wa mshambuliaji huyo amesema familia ya Messi ilitaka kuonyesha uwazi, na hali ya ushirikiano na sasa mambo yamekwenda sawa.

Kama atapatikana na hatia Messi na babake wanaweza kutozwa faini ya hadi asilimia 150 ya kiasi cha fedha wanachodaiwa kama deni. Inadaiwa walipata faida kubwa na wakakwepa kulipa kodi kwa kutumia makampuni ya ng'ambo kama vile Uruguay. Wote wawili wanakanusha madai hayo na hata kuungwa mkono na rais wa Barcelona Sandro Rosell na rais wa zamani Joan Laporta.

Babake Messi alifanya malipo ya zaidi ya euro milioni 5 mnamo Agosti 14 kugharamia madai hayo ya madeni ya kodi na riba. Malipo hayo yaliifanya mahakama kuamua kuwa Messi na babake hawakustahili kuwasilisha ombi la dhamana. kesi hiyo hata hivyo haijamzuia Messi dhidi ya kufanya kazi yake. Kwa sasa anaongoza katika ufungaji wa mabao mengi katika Laliga akiwa na mabao saba msimu huu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Josephat Charo