1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Messi ndiye mfalme wa kandanda duniani

12 Januari 2016

Mshambuliaji wa klabu ya kandanda ya Barcelona, na timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi, amenyakuwa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ulimwenguni. Hii ni tuzo yake ya tano ya Ballon d'Or

https://p.dw.com/p/1Hbi6
Schweiz, Ballon d'Or Gala 2015 Lionel Messi
Picha: picture-alliance/dpa/A. Wiegmann

Messi aliwapiku Christiano Ronaldo anayeichezea timu ya taifa ya Ureno na kilabu ya Real Madrid na Neymar mchezaji wa timu ya Brazil na kilabu ya Barcelona. Messi sasa ameweka rekodi kwa kushinda tuzo hiyo ya shirikisho la soka duniani FIFA Ballon d'Or kwa mara ya tano

Messi mwenye miaka 28 alipata asilimia 41.33 ya kura zote zilizopigwa, huku Cristiano Ronaldo akishika nafasi ya pili kwa asilimia 27.76 ya kura n Neymer akipata asilimia 7.86.Tuzo hiyo katika miaka ya karibuni imegeuka kuwa kinyang'anyiro cha kibinafsi kati ya Messi na Ronaldo. Muargentina Messi, ambaye amekuwa katika orodha ya tatu bora mwaka wa tisa mfululizo, pia alishinda tuzo hiyo mara nne mfululizo baina ya 2009 na 2012, huku Mreno Ronaldo akiishinda mara tatu, mara moja akiwa katika klabu ya Manchester United mwaka wa 2008 na mbili akiwa na Real Madrid. Mara pekee katika miaka saba iliyopita ambapo Messi na Ronaldo hawakupata nafasi mbili za kwanza ni 2010 wakati wachezaji watatu wa Barca; Messi, Andres Iniesta na Xavi waliteuliwa pamoja.

Kwa upande wa wanawake nyota wa Marekani Carli Lloyd, ameibuka kuwa mchezaji bora wa mwaka wa 2015.

Goli bora la mwaka likifahamika kama Puskas limwendea Wendell Lira anayecheza katika Atletico Goianiense ya Brazil.

Kocha wa Barcelona Muhispania Luis Enrique amechaguliwa kuwa kocha bora wa mwaka kwa kuiongoza Barca kutamba barani Ulaya kwa kutwa mataji matano msimu uliopita. Enrique aliwabwaga Pep Guardiola wa Bayern Munich na Jorge Sampaoli wa Chile.

Jill Ellis kocha wa kikosi cha taifa cha Marekani amekuwa kocha bora wa wanawake baada ya kuongoza timu ya taifa ya Marekani kufanya vyema katika michuano ya kombe la dunia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga