1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah afariki dunia

Iddi Ssessanga
29 Septemba 2020

Mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah al-Ahmad Al-Saba, alieunda sera ya sasa ya taifa hilo na mpatanishi katika baadhi ya mizozo mibaya zaidi ya kanda ya Ghuba amefariki dunia siku ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 91.

https://p.dw.com/p/3jBfE
Kuwait Emir Sheikh Sabah al-Ahmad Al-Sabah
Picha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Sheikh Saba alijipatia sifa kama kiongozi shupavu na asietikisika, ambaye aliisaidia nchi yake kupita katika uvamizi wa Iraq wa mwaka 1990, mporomoko wa masoko ya mafuta na machafuko katika bunge na mitaani.

"Kwa huzuni na majonzi, tunaomboleza kifo cha Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber Al-Sabah," alisema Sheikh Ali Jarrah Al-Sabah, waziri wa masuala ya ufalme, katika hotuba iliyotolewa kwa njia ya televisheni.

Serikali baadae ilitangaza kuwa taifa litaingia katika kipindi cha maombolezo cha siku 40. Mfalme huyo, alielitawala taifa hilo tajiri kwa mafuta tangu 2006, amefariki nchini Marekani ambako alikuwa akitibiwa, baada ya kufanyiwa upasuaji katika mji wa Kuwait City. Taarifa za kina kuhusu ugonjwa wake hazikutolewa.

Kuwait Scheich Nauaf al-Ahmad al-Sabah
Mfalme mpya wa Kuwait Sheikh Nawaf Al-Ahmad al-Sabah.Picha: Yasser Al-Zayyat/AFP

Wakati akiwa hayupo, Sheikh Nawaf -- mmoja wa viongozi wakuu wa serikali ambaye ameshikilia nyadhifa za juu kwa miongo kadhaa, zikiwemo wizara za ulinzi na mambo ya ndani -- amekuwa akikaimu nafasi ya mfalme.

Soma pia: Juhudi za Kidiplomasia zachachamaa Ghuba

Kiongozi wa 15 katika familia ambayo imetawala Kuwait kwa zaidi ya miaka 250, Sheikh Sabah amemudu mizozo ya Kuwait kwa kufanya maamuzi ya uerevu na kutumia mkono wa chuma.

Kama mwanadiplomasia wa juu wa taifa hilo kwa karibu miongo minne, aliendeleza mahusiano ya karibu na mataifa ya magharibi, hasa Marekani ambayo iliongoza muungano wa kimataifa ulioikomboa Kuwait kutokana na ukaliaji wa Iraq mwaka 1991.

Baadae aliibuka kama mpatanishi kati ya Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba na Iran, na kati ya Saudi Arabia na Qatar, kufuatia uamuzi wa Riyadh mwaka 2017, kukata mahusiano na Doha.

Golf Kooperationstreffen Council
Mfalme Salma wa Saudi Arabia (wa pili kutoka kulia), akiwa ameshikana mikono na marehemu Sheikh Sabah waakti mkutano wa pembeni wa Baraza la Ghuba mjini Royadh, Saudi Arabia, Desemba 9, 2018.Picha: picture-alliance/AP Photo

Katika ishara ya heshima aliokuwa nayo mfalme huyo ndani ya migawanyiko ya kisiasa ya kanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Qatar zimetangaza siku tatu za maombolezo.

Kiongozi mwenye busara

"Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu yamepoteza mmoja wa viongozi wake muhimu," alisema rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi katika ujumbe wa Twitter.

Bahrain ilisema kwamba Kuwait imempoteza "kiongozi mwenye busara, amir wa binadamu aliependa kilicho bora kwa ajili ya watu."

Soma pia: Wafadhili wakutana Kuwait kuichangia Syria

Pande zinazohasimiana nchini Yemen pia zimetoa heshima pia. Msemaji wa kundi la waasi wa Kihouthi alitweet kuwa waasi "hawatosahau--mapenzi yake kwa Yemen na umakini wake wa kuzima moto wa vita."

Serikali mjini Baghad ilisema Sheikh Sabah alikuwa ameuweka ukaliaji wa Iraq katika wakati uliyopita na kuunga mkono Iraq "mpya" baada ya kuondokana na utawala wa Saddam Hussein, akichagua kusimama na taifa hilo dhidi ya "ugaidi".

China Peking treffen mit Vertretern arabischer Staaten
Sheikh Sabah akisalimiana na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing, Julai 9, 2018.Picha: Reuters/A. Wong

Kiongozi huyo wa Kuwait aliendelea kujihusisha kwa undani katika masuala ya kidunia hadi umri wake wa uzeeni.

"Kifo cha Sabah al-Ahmed kitagusa sana, kutokana na umashuhuri wake kama mwanadiplomasia na mpatanishi wa kikanda na kama kiongozi muunganishaji nyumbani," alisema Kristin Diwan wa taasisi ya Mataifa ya Ghubaya Kiarabu mjini Washington.

Soma pia:KUWAIT Mwanamke wa kwanza ateuliwa kuwa waziri

"Wakuwait wamekubali uwezo wake wa kuweka nchi hiyo nje ya mizozo ya kikanda na uhasama."    

Hakutarajiwi mabadiliko ya kisera kwa mtawala mpya

Mabadiliko makubwa ya kisera hayajatarajiwi chini ya mrithi wake, hata baada ya kanda ya Ghuba kupitia mabadiliko makubwa ambapo majirani wa Kuwait, UAE na Bahrain, yaliamua kuanzisha uhusiano na Israel.

Kuwait Geberkonferenz Wiederaufbau Irak
Mmoja ya mikutano ya wahisani uliyofanyika Kuwait chini ya uenyekiti wa mfalme Sheikh Sabah.Picha: Reuters/S. McGehee

"Uongozi wa Kuwait utatoa kipaumbele kwa utulivu wa ndani ya nchi na katika siasa za kikanda. Msisitizo utakuwa kwenye utulivu wa ndani," alisema Diwan.

Soma pia:Wafadhili waichangia Syria dola bilioni 2.4

"Kutakuwa na mengi ya kusimamia ndani ya nchi wakati ambapo uchaguzi wa bunge ukitarajiwa katika muda wa miezi miwili ijayo."

Kuweka sawa uhusiano na Israel ni jambo linalochukiwa sana nchini Kuwait, ambayo kwa sehemu kubwa inaunga mkono msimamo wa kihistoria wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, wa kudai azimio linalounga mkono harakati za Wapalestina kabla muafaka wa kidiplomasia na Israel.

"Hakuna ishara kwamba uongozi wa baadae utataka kubadili msimamo wa Kuwait," Diwan alisema.

Washambulizi wa London watambulishwa

Katiba ya Kuwait inainisha kuwa mfalme anapaswa kutoka kwenye kizazi cha mwasisi wa taifa hilo, Mubarak al-Sabah, lakini kiti cha ufalme kimezunguka miongoni mwa vizazi vya watoto wake, Salem na Jaber, kwa miongo minne.

Soma zaidi: KUWAIT:Wafungwa 5 wa Guantanamo wapelekwa nyumbani

Wagombea wa nafasi ilioachwa na mrithi wa kiti cha ufalme wanajumuisha mtoto wa Sabah na naibu waziri mkuu wa zamani na nguli wa siasa Nasser Sabah al-Ahmad.

"Sheikh Nawaf Al-Ahmaed anapaswa kutazamwa zaidi kama msimamizi kuliko kiongozi mpya," alisema Cinzia Bianco, mtafiti katika Baraza la Ulaya kuhusu mahusiano ya kigeni.

"Nyuma ya pazia hata hivyo, wanamfalme vijana wana uwezekano wa kuendelea kushindana ili kumrithi.

Chanzo: AFPE